UKURASA WA 921; Hakuna Ubaya Kwenye Kutaka Zaidi…

By | July 9, 2017

Kuna namna jamii inayotuzunguka inajaribu kuturudisha nyuma, na njia hii imekaa kisaikolojia zaidi hivyo wengi hawaioni.

Njia hii ni kufanya kutaka zaidi kuonekane ni kubaya, kuonekane ni tamaa, ni roho mbaya. Kwa nini usiridhike na kidogo ulichopata! Hivi ndivyo jamii inajaribu kutuhadaa tusitake makubwa zaidi, tusipambane na tuishie kuwa kama kila mtu.

Ukweli ni kwamba, hakuna ubaya wowote kwenye kutaka zaidi, kama unataka zaidi kwa njia sahihi. Tena kutaka zaidi kwa njia sahihi, kuna manufaa makubwa zaidi kwa jamii nzima.

Kwa mfano, kama unataka kutengeneza kipato zaidi, kwa kuongeza thamani zaidi kwenye biashara yako, thamani hiyo inaenda wapi? Si ni kwenye jamii? Kama unataka kutengeneza kipato zaidi kwa kuongeza biashara au bidhaa zaidi, anayenufaika ni nani? Si jamii?

Sasa shangaa kwa nini jamii hiyo hiyo inakuwa ya kwanza kukuambia usitake zaidi, kuwa kama wengine, ridhika na unachopata. Nikupe siri kwamba jamii inafanya hivyo ili usioneshe uzembe wako.

SOMA; Wenye Uhitaji Zaidi Ndiyo Wasiotaka…

Chukua mfano, umeajiriwa sehemu ambayo umekuta watu wako pale zaidi ya miaka kumi. Wewe ukaenda na kuyasoma mazingira, ukaona kuna namna sehemu ile inaweza kunufaika zaidi kwa uwepo wako. Ukaandaa mpango ambao utaweza kufanya vitu zaidi na kipato chako kiongezwe. Unafikiri watu wale watapokeaje mapendekezo yako? Lazima wayapinge, lazima waoneshe haiwezekani. Kwa sababu hilo likiwezekana, basi wao wamekuwa wazembe kwa miaka kumi waliyokuwa pale. Hakuna anayependa aibu hiyo.

Hivyo rafiki, taka kupata zaidi ya unachopata sasa, lakini tumia njia sahihi kupata hicho zaidi. Tegemea upinzani na vikwazo kutoka kwa wengine, lakini hilo lisikurudishe nyuma. Hakuna ubaya wowote kwenye kutaka zaidi, iwapo kila mtu atanufaika. Ila kuwa macho na wale ambao hawatafurahishwa na hilo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.