UKURASA WA 920; Ukweli Haumbadilishi Mtu Huyu…

By | July 8, 2017

Moja ya vitu unapaswa kuelewa kwenye maisha yako, ili uweze kuokoa muda na nguvu zako ni kwamba kuna watu hawawezi kubadilishwa, hata ungewapa ukweli kiasi gani. Wapo watu ambao watakataa au kupinga jambo, watakukataa au kukupinga kwa lolote, na huna namna unaweza kufanya kuwabadili.

Hata ukiwapa ukweli, ukiwapa taarifa sahihi zinazoonesha wako upande ambao siyo sahihi, bado hawatabadilika. Kwa kifupi ndivyo walivyo na chochote utakachowaambia watatafuta namna ya kukipinga au kuwa na wasiwasi nacho.

Leo nakukumbusha hili, ili uokoe muda na nguvu zako, hasa pale unapotaka kuwadhibitishia watu kwamba wanakosea. Wengi hawatakubaliana na wewe, kwa sababu ni wachache sana ambao wanapenda kukiri wamekosea au wapo upande ambao siyo sahihi.

Na hapo bado kuna swala la imani, iwapo mtu anaamini tofauti na kile unafanya wewe, hakuna kiwango cha ukweli utakachompa aweze kukubaliana na wewe. Yeye ataendelea kuamini kile anachoamini, licha ya juhudi utakazofanya kumbadilisha.

SOMA; Kuhodhi Ukweli…

Watu wa aina hiyo, huja kubadilika wao wenyewe, baada ya uzoefu wao wenyewe, kutokana na kukosa walichotaka kwa kukaa upande uliokuwa siyo sahihi, au kujaribu na kuona matokeo mazuri.

Hivyo, kama kuna mtu ambaye ungetamani sana abadilike, kwa manufaa yake, kitu pekee unaweza kumsaidia ni kumpa nafasi ya kupata uzoefu yeye mwenyewe. Iwe ni uzoefu wa kunufaika au uzoefu wa hasara na kuumia. Hapo ataondoka na funzo muhimu litakalomfanya kuchukua hatua.

Ukweli hauwabadilishi watu ambao hawataki kubadilika, bali uzoefu wanaoweza kuupata ndiyo utawabadili.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.