UKURASA WA 932; Ukimya Na Kujidhibiti…

By | July 20, 2017

Ni silaha muhimu sana kwako katika zama hizi tunazoishi.

Kwa sababu zimekuwa zama ambazo kila mtu anaweza kutoa maoni yake kwenye kila jambo, kila mtu anaweza kukosoa, kila mtu anaweza kulalamika. Na ni rahisi vitu hivyo kuwafikia wengi kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa kuwa unaweza kufanya hivyo, na kwa sababu kila mtu anafanya, haimaanishi na wewe ufanye. Kwa sababu mengi utakayojihusisha nayo, kwa kutoa maoni, kukosoa au kulalamika, hayatakuwa na msaada wowote kwako na wala hayatamsaidia yeyote. Na kwa bahati mbaya sana, wanaweza kueleweka vibaya na kukuingiza kwenye matatizo na wengine.

Hivyo dawa pekee ni ukimya na kujidhibiti wewe mwenyewe.

Kuwa kimya, usikimbilie kuongelea kila kitu, usikimbilie kujibu kila unachoulizwa, usikimbilie kukosoa kila unachoona. Kumbuka kukaa kwako kimya kutakusaidia mengi, kwanza utajifunza na pili, utajiepusha na matatizo ya wengine.

SOMA; Tabia Moja Itakayokuwezesha Kudhibiti Matumizi Ya Fedha Zako.

Kujidhibiti wewe mwenyewe ni muhimu kwa sababu kukaa kimya kunaweza kukawa na ukomo. Ukapata msukumo mkubwa kutoka ndani yako, kwa kuona siyo sahihi jambo liende kama linavyoenda, wakati wewe unaweza kusema na kufanya kitu. Hapa ndipo unapaswa kujidhibiti, ili hatua unayochukua iwe ya msaada kweli.

Katika kujidhibiti jiulize swali hili muhimu; je hichi ni kitu ambacho nataka kweli kusema? Au nasema tu ili na mimi nisikike? Kama ni kitu muhimu kweli, na unaweza kusaidia basi sema na fanya. Lakini kama umejikuta unataka kusema na kufanya kwa sababu tu kila mtu anafanya hivyo, acha mara moja.

Ukimya na kujidhibiti mwenyewe, kutakusaidia kuondokana na changamoto zisizo za lazima katika enzi hizi za kelele za kila aina.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.