UKURASA WA 935; Mapenzi Yanapotawala Maamuzi, Ndiyo Chanzo Cha Maafa…

By | July 23, 2017

Hisia na fikra huwa zinaenda kinyume, hisia zikiwa juu, fikra zinakuwa chini. Hii ndiyo sababu watu wote wanaofanya maamuzi wakiwa na hisia kali, kama za furaha au hasira, huja kujutia maamuzi yao, mara zote. Kumbuka kama hujawahi kufanya maamuzi ukiwa na hasira, lakini baada ya hasira kuisha, ukatamani usingefanya maamuzi hayo. Au fikiria kama hujawahi kuwa na furaha sana, ukaahidi kitu fulani, ambacho baada ya furaha ile kuisha, ukatamani usingeahidi.

Sasa kuna upofu mwingine mkubwa sana kwenye kufanya maamuzi sahihi. Upofu huu unatokana na mapenzi. Mtu akishakipenda kitu kweli, atatafuta kila njia ya kukitetea, kuonesha kwamba ni sahihi. Hata kama siyo sahihi, na kila mtu anaona siyo sahihi, kwa mapenzi yake binafsi, ataendelea kuona ni sahihi.

Hilo lilikuwa likionekana kwenye upande wa mahusiano, ambapo kijana anampenda mtu ambaye wengine wanaona siyo sahihi kwake, lakini hasikii kabisa.

Sasa hivi hilo limekuwa hatari zaidi kwenye maisha ya kazi na biashara. Watu wanapenda vitu ambavyo siyo sahihi, lakini huwezi kuwaambia lolote wakakuelewa. Kwa mfano zipo fursa za kutengeneza fedha zama hizi, nyingi kati ya hizo siyo sahihi, kwa sababu zinakuwa hazina msingi sahihi wa kiuchumi. Lakini watu wanazijaribu na wakipata fedha, mapenzi yao yote yanaenda kwenye fursa hizo, na hawaoni hatari inayokuwa ipo mbele yao. Wanaruhusu mapenzi juu ya fursa zile yawatawale, halafu hilo linawapelekea kufanya maamuzi mabovu.

SOMA; Haya Ndio Maafa Unayojitengenezea Mwenyewe.

Hivyo rafiki, pale unapoona watu wanatoa walakini juu ya kitu fulani, ambacho wewe unakiamini na kukipenda, usiishie kuwakatalia, badala yake jipe muda wa kuchunguza kwa undani zaidi. Jifunze kuona wapi msingi sahihi ulipo. Na unahitaji kuwa makini sana hapa kwa sababu unaweza kuishia kutafuta kile kinachounga mkono msimamo wako. Unapaswa kupata taarifa sahihi kutoka pande zote mbili, upande unaoamini wewe na upande unaopinga kile unachoamini. Kisha jua msingi upo wapi na fanya maamuzi yako kwa kufuata msingi.

Usiruhusu mapenzi yako juu ya kitu au jambo lolote yakupe upofu wa kushindwa kuona mambo yaliyo wazi kabisa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.