UKURASA WA 936; Tatizo Ni Kutafuta Furaha Sehemu Ambapo Haiwezi Kupatikana…

By | July 24, 2017

Watu wengi wamekuwa wanaihusisha furaha na mafanikio, lakini siyo mafanikio kama mafanikio, bali mafanikio ya vitu, fedha, mali na kadhalika. Na hapo ndipo utawasikia wengi wakisema fedha hazileti furaha, au utajiri hauleti furaha, au mali hazileti furaha. inakuwa sahihi kabisa kwa sababu watu wanakuwa wanafanya kosa la kutafuta furaha sehemu ambapo hawawezi kuipata.

Mtu ambaye hajawahi kula mkate kabisa, mpe mkate kwa mara ya kwanza, ataufurahia sana. Ataona ni kitu kizuri na cha kipekee. Endelea kumpa mkate kila siku, ataanza kuuchoka, na kuona kitu cha kawaida, na hapo ataanza kutaka vitu zaidi, labda mkate wa siagi, au maziwa, au mayai.

Hivyo ndivyo binadamu tulivyo kwenye vitu, kitu kipya kwetu tunakipenda na kukifurahia kwa muda, lakini kadiri muda unavyokwenda, tunakizoea na kukiona cha kawaida. Ile hamasa yetu ya mwanzo inatoweka, na tunaanza kutafuta kitu kingine zaidi.

Siyo jambo baya kutaka zaidi, ni asili yetu binadamu na ndiyo inafanya tufanikiwe na kuweza kufanya makubwa kimaisha.

SOMA; Jinsi ya kushinda hali ya kutokuwa na furaha.

Hatari kubwa ipo pale tunapoihusisha furaha kwenye hilo. Hapo ndipo tunapoishi maisha ya kupanda na kushuka, tunakuwa kama tunakimbiza upepo, hatuushiki, licha ya kuweka juhudi kubwa kukimbiza.

Furaha haipaswi kuunganishwa na kitu chochote, haipaswi kuwekwa pembeni mpaka tupate kitu fulani. Furaha ni kitu ambacho tunapaswa kwenda nacho, kwenye kila hatua ya maisha yetu. Kwa kujikubali vile tulivyo, kuyapenda maisha yetu na kutoa mchango mkubwa kwa wengine.

Hutafuti mafanikio ili uwe na furaha, bali unakuwa na furaha ili ufanikiwe. Furaha inaleta mafanikio, na usijichanganye ukitaka kufanikiwa ndiyo ufurahi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.