UKURASA WA 939; Sikiliza Zaidi Ya Unavyoongea…

By | July 27, 2017

Mwanasaikolojia mmoja amewahi kusema, watu hawawezi kuficha siri. Kama ataficha kwa maneno, basi matendo yake yataonesha. Kama atajipanga asionekane hata kwa matendo, basi hata sauti yake itaonesha siri inayofichwa.

Lakini huwezi kujua hayo, kama hujui jinsi ya kuyajua. Na jinsi pekee ya kujua hayo mazito, ni kusikiliza zaidi ya unavyoongea.

Mfano ambao umekuwa unatumiwa sana ni kwamba tumepewa masikio mawili na mdomo mmoja, ili tusikilize zaidi ya tunavyoongea. Una ukweli mkubwa sana usemi huo, kwa sababu unapofanya hivyo, unajifunza mengi sana.

Nataka nikuongezee kitu kimoja zaidi, sikiliza kwa masikio na kwa macho pia. Unapomwangalia mtu anayeongea, yapo mengi ambayo unayapata kuliko usipomwangalia.

Unaposikiliza zaidi ya unavyoongea, unajifunza mambo mengi, mambo ambayo ulikuwa huyajui. Kwa sababu unapoongea hakuna kipya unachojifunza, unatoa kile ambacho kipo ndani yako. Lakini ukisikiliza, unajifunza mambo mapya kutoka kwa wengine.

SOMA;  Watu Wanakuangalia Zaidi Ya Kukusikiliza….

Ukisikiliza kuliko kuongea pia unaboresha mahusiano yako na wengine. Hakuna kipindi ambacho kusikiliza ni dili kama sasa. Kwa sababu zama hizi kila mtu anataka kusema, na kila mtu anataka kusikika, hakuna aliye tayari kukaa na kusikiliza kweli. Watu wanasikiliza siyo kuelewa, bali wanasikiliza huku wanafikiria cha kujibu. Hivyo ukiwa na utaratibu wa kusikiliza kweli, kwa makini, unawaelewa watu na wanafurahia pale unapowaelewa, na kukupenda pia.

Unaposikiliza zaidi ya kuongea, unaepuka kufanya makosa yasiyo ya lazima. Hakuna mtu amewahi kukosea kwa kukaa kimya, lakini tunawaona wengi wakikosea kwa kuongea hovyo, au kuongea na wakaeleweka vibaya.

Unaposikiliza zaidi ya kuongea, unajijengea nidhamu, unajijengea uvumilivu na kuwa na subira. Kwa sababu kila mtu anakimbilia kuongea na yeye asikike, wewe ukiweza kukaa kimya na kusikiliza, utakuwa na nidhamu nzuri.

Kwa vyovyote vile, sikiliza zaidi ya unavyoongea, wape watu nafasi ya kuongea, sikiliza kwa makini, elewa kisha zungumza yale ambayo ni muhimu pekee. Kwa njia hii utaheshimiwa na kupendwa pia kwa sababu utawaelewa watu vizuri, na kuwasaidia kwa namna bora kwao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.