UKURASA WA 963; Epuka Kununua Matatizo Ya Wengine…

By | August 20, 2017

Pamoja na maisha kuwa magumu na yenye changamoto nyingi, bado sisi wenyewe tumekuwa tunatafuta ugumu na changamoto zaidi.

Na sehemu ambayo tumekuwa tunafanya hivyo ni kwenye kununua matatizo ya wengine. Au kama ninavyopenda kuliita hili, kuchomeka pua yako kwenye matatizo ya wengine.

Ipo kauli moja ya kiingereza inasema MIND YOUR OWN BUSINESS, ikiwa na maana kwamba jali mambo yako. Hii ni kauli yenye nguvu sana, kwa sababu unapojali mambo yako, na ukawaacha wengine wajali mambo yao, utapunguza nusu ya changamoto na matatizo uliyonayo sasa.

Huenda unajiuliza umekuwa unanunuaje matatizo ya wengine, huenda unafikiri kwamba wewe unajali yako. Lakini hebu tuangalie haya matatu muhimu ambayo watu huwa wanapenda kuyafanya, na uone kama na wewe huyafanyi.

  1. Kutoa ushauri ambao hujaombwa.

Au hata kutoa maoni wakati hakuna aliyekuomba maoni yako. Hii ni njia ambayo wengi wamekuwa wanaitumia kununua matatizo ya wengine. Kwa sababu watu huamini wanajua zaidi ya wengine, na kuona maoni yao ni muhimu na yatasaidia.

Lakini nikuhakikishie kitu kimoja, kama mtu hajaja kwako na kukuomba ushauri au maoni, ushauri au maoni yoyote unayompa yeyote, unapoteza muda wako, na kutafuta matatizo zaidi. Kwa sababu hayatafanyiwa kazi, na zaidi yanaweza kutafsiriwa vibaya na ukaonekana wewe ndiyo mbaya.

SOMA; Chimbuko La Matatizo Yote Ya Binadamu….

Kama hujaombwa ushauri, ni vyema ukakazana na yako. Na siyo kila jambo linahitaji maoni yako, acha mengi yapite, dunia itaenda vizuri tu bila ya neno lako.

  1. Majungu na umbeya.

Njia nyingine ambayo watu wamekuwa wanaitumia kununua matatizo ya watu ni kujihusisha na majungu na umbeya. Pale unapoambiwa mambo ya watu na wewe kuyasambaza, unakuwa umechagua kununua matatizo ya watu hao. Ukishaingia kwenye majungu tu, tayari umeshakuwa sehemu ya tatizo. Na maneno ya majungu huwa yanazunguka mpaka yanamfikia mhusika, halafu yanaanza kurudi kumpitia kila ambaye amehusika kwenye mlolongo huo wa majungu.

Epuka sana kuhusishwa na majungu, mtu anapokuja kukuletea habari kuhusu mtu fulani, mwulize kwa nini asiende kumwambia mwenyewe? Au kama inawezekana mwambie asubiri mumwite mhusika. Kwa njia hii watakuona wewe siyo wa majungu na watakuondoa kwenye mduara wa majungu.

Kama imetokea umesikia majungu au umbeya juu ya mtu fulani, basi hayo yaishie kwako, usiyapeleke kwa mtu mwingine yeyote. Hata kama ni ile ya …. umesikia…. acha kabisa. Mambo ya aina hiyo huwa hayaishi vizuri.

  1. Kumsema mtu ambaye hayupo.

Hii inafanana kidogo na majungu, lakini wakati mwingine inaweza isiwe majungu. Labda mmekaa mnaongea na kupiga soga, ghafla hadithi zinahamia kwa mtu ambaye hayupo kati yenu. Watu wanaanza kuchangia, lakini fulani bwana…. huenda yanayosemwa wala hata siyo mabaya, lakini kumbuka yeye hayupo, hivyo neno lolote unalosema, linaweza kutafsiriwa vibaya na wengine halafu likafikishwa kwake kwa maana tofauti na uliyosema wewe.

Ataenda kuambiwa, halafu fulani alisema hivi kuhusu wewe…. hapo sasa ndiyo ataanza kujiuliza ilikuwaje mpaka mnamjadili wakati yeye hakuwepo pale.

Acha mara moja kununua matatizo ya wengine, na ninakuhakikishia, utakapoanza kujali mambo yako, ukikazana kuyafanya maisha yako kuwa bora, huwezi kupata kabisa muda wa kufuatilia mambo ya wengine. Labda kama wao wenyewe wamekuomba msaada wa moja kwa moja. Tofauti na hapo, ukijiona wewe ndiyo unajua mambo ya kila mtu, ya kweli na ambayo siyo ya kweli, hebu jiulize una kitu chochote kikubwa unapigania kwenye maisha yako kweli?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.