UKURASA WA 970; Hamasa Haisubiriwi, Hamasa Inatengenezwa…

By | August 27, 2017

Hivi unafikiri mti wa mwembe huwa unatoa miembe wakati una hamasa au unatoa miembe kwa sababu ndiyo kazi yake? Vipi kuhusu viumbe wengine tunaoishi nao hapa duniani? Unafikiri kwamba wanakaa na kuona sasa nina hamasa basi acha nifanye kazi yangu?

Jibu ni hapana, kila kiumbe kinatimiza wajibu wake hapa duniani, kwa sababu ndiyo wajibu wake. Kuna swala la muda na majira lakini yote hayo ni katika mipangilio na asili ya kila kiumbe hai. Lakini hutakutana na kiumbe hai ambacho kinaacha kufanya kitu kwa sababu hakina hamasa, ila tu binadamu.

Watu wamekuwa wanaanza kufanya vitu vikubwa na kuishia njiani. Wengine wanashindwa kabisa kuanza. Na kikubwa kinachowazuia ni hamasa. Wengi wanakuwa hawana hamasa kabisa ya kuwasukuma kuanza kufanya. Wengine wanakuwa na hamasa kidogo ambayo baada ya muda inapotea na hivyo kuacha kufanya.

Kama bado upo kwenye kufikiri kuhusu hamasa, kuna uwezekano wa mambo haya mawili;

Moja labda bado hujajua wajibu wako hapa duniani ni nini. Na hii ni hasara kubwa sana kwa sababu bila ya kujua wajibu wako hapa duniani, unawasindikiza wengine kwenye kutimiza wajibu wao, na mbaya zaidi watakutumia wewe kufikia wajibu wao.

Mbili unajaribu kutoroka wajibu wako, hapa umeshaujua, lakini unataka kuutoroka, hutaki kutekeleza wajibu wako, kwa sababu ya uvivu na uzembe.

Lakini yote kwa yote, hamasa haipaswi kuwa kitu kinachokuzuia wewe kufika pale unapotaka kufikwa. Kwa sababu hamasa siyo kitu ambacho kinasubiriwa, bali ni kitu ambacho kinatengenezwa.

Hata usubiri hamasa kwa muda mrefu kiasi gani, huwezi kuipata, siyo kwa sababu hamasa haikuoni wewe, bali ni kwa sababu hamasa haipo kukusubiri wewe.

Hamasa inatengenezwa, na inatengenezwa kwa kufanya. Unapofanya, unapotekeleza wajibu wako, hapo ndipo unapotengeneza hamasa. Pale unapoona unafanya kitu, unazalisha matokeo, unaongeza thamani kwa wengine, hapo ndipo unapotengeneza hamasa, ambayo inakusukuma wewe kuchukua hatua zaidi.

Kusubiri hakuwezi kuleta hamasa ya aina yoyote ile. Hata kuwaangalia wengine, kama kutaleta hamasa ni ya muda tu, haiwezi kudumu muda mrefu.

Sawa na moyo ambao unawashwa na njiti ya kiberiti, ili uendelee kuwaka lazima uendelee kuwaka. Ukiacha kuwaka unazima.

Hivyo na kwenye hamasa, kama kuna chochote cha nje ambacho kinaweza kutupa hamasa basi ni kama cheche tu inayoanzisha moto. Lakini ili moto uendelee kuwaka, lazima uendelee kuwaka.

Ili uendelee kuwa na hamasa na kile unachofanya, lazima uendelee kufanya kile unachofanya. Acha kufanya na hamasa inapotea.

Hivyo basi, chochote unachopanga kufanya, chochote ambacho ulianza kufanya ila ukaishia njiani, dawa ni moja, endelea kufanya. Fanya ukijua kwa nini unafanya, fanya ukilenga kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Na utapata hamasa kubwa ya kuendelea kufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.