UKURASA WA 971; Ubaya Ni Pale Vinapotokea Kidogo Kidogo…

By | August 28, 2017

Vitu ambavyo vinatokea kwa mara moja, labda kinaharibika chote kwa mara moja, au kitu kinavunjika mara moja, siyo tatizo kubwa, kwa sababu unaona kimevunjika au kuharibika na kuchukua hatua.

Tatizo kubwa lipo kwenye vitu ambavyo vinaharibika kidogo kidogo, taratibu taratibu. Hivi huwa tatizo kubwa na kuleta madhara makubwa. Hii ni kwa sababu mtu huchelewa kuchukua hatua, huona bado tatizo siyo kubwa sana na kuchelewa kuchukua hatua. Pale anapoona tatizo limekuwa kubwa, linakuwa halifai tena kurekebisha kwa hatua anazoweza kuchukua.

Tunaweza kuona mifano mingi kwenye kila eneo la maisha yetu;

Tukianza na afya, mtu anapopata changamoto kubwa, labda ameumia au amepata ajali, huchukua hatua haraka kunusuru afya yake. Lakini pale ugonjwa unapokuwa kidogo kidogo, ni kichwa kinauma kidogo kila siku, au kikohozi cha kawaida lakini hakiishi, au kauvimbe kadogo lakini hakaumi. Haya ni rahisi kuyachukulia kuwa ni ya kawaida, ila siku inapofika na kujikuta huwezi kuvumilia tena, ndiyo inagundua ulishachelewa kuchukua hatua.

Kwenye biashara pia hili lipo wazi kabisa, ikitokea hasara kubwa ya mara moja kwenye biashara, utakimbilia kuchunguza na kuchukua hatua mara moja. Lakini pale hasara zinapokuwa ndogo, elfu moja leo, elfu mbili kesho, ni rahisi kuchukulia kawaida, mpaka pale unapokuja kustuka hasara hizi zimekuwa kubwa na biashara inaelekea kufa.

SOMA; Tabia Moja Inayowaingiza Watu Wengi Kwenye Madeni Ya Kifedha, Na Namna Ya Kuiepuka.

Tunaweza kuona hili kwenye ajira pia, mtu akifukuzwa kazi mara moja atakazana kuchukua hatua. Lakini kazi inapokuwa inapotea kwake taratibu, kuna kila dalili kwamba kazi hiyo haitadumu, haoni na kuchukua hatua.

Hili linatukumbusha umuhimu wa sisi kujua wakati sahihi wa kuchukua hatua. Na wakati sahihi ni pale ambapo tunaona mambo ambayo hayaeleweki, hata kama ni madogo kiasi gani.

Tusichukulie jambo lolote kwa urahisi, kila kitu tukichunguze kwa undani. Hakuna kitu kinachotokea tu kwa bahati mbaya, kila kitu kinatengenezwa, kila kitu kinasababishwa.

Tunapoona mabadiliko yoyote kwenye afya zetu, mahusiano yetu, kazi zetu na hata biashara zetu, tunapaswa kwenda ndani zaidi na kuhakikisha tunaelewa kwa hakika nini hasa kinaendelea.

Na ujanja zaidi ni kuwa mbele ya kila ambacho kinaweza kutokea. Kwa kutabiri wewe mwenyewe, kutengeneza kila aina ya uwezekano wa vitu kutokea, kisha kujilinda visitokee.

Tunapoona mambo madogo madogo na kusubiri tukiamini ni madogo na yatapita tu, hapo ndipo tunapotoa mwanya wa mambo kuwa makubwa na kushindikana kuyabadili. Wakati wa kuchukua hatua ni pale unapoona chochote cha tofauti.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.