UKURASA WA 974; Vitu Vidogo Vinapokosekana, Vinaharibu Sifa Na Ladha Nzima…

By | August 31, 2017

Kupika chakula chochote ni zoezi gumu, linalohitaji akili, nguvu na subira kuhakikisha unapata chakula kizuri kwa ajili ya kula. Zoezi la kuweka chumvi kwenye chakula ni rahisi, halihitaji nguvu na maarifa mengi kama ilivyo kwenye kupika.

Lakini kazana kupika chakula chako vizuri mno na sahau kuweka chumvi, chakula kinakosa ladha. Kazi yote ya kupika inakuwa imekosa maana kwa kushindwa tu kuweka chumvi, kitu ambacho hakihitaji nguvu kubwa au akili kubwa.

Huu ni uhalisia wa maisha yetu, hasa kwenye shughuli ambazo tumechagua kufanya. Iwe ni kazi au biashara, kuna vitu vinatuhitaji nguvu na akili zetu, lakini vipo vingine ni rahisi, lakini vinapokosekana vinaharibu kazi kubwa iliyowekwa.

Kwa mfano unaweza kukazana sana kuweka juhudi kubwa kwenye kile unachofanya, ukaweka juhudi usiku na mchana, ukawa mbunifu wa kipekee, lakini ukakosa uaminifu. Hilo pekee linaharibu kabisa kazi zote kubwa unazofanya. Ni kweli watu wanataka kazi zako nzuri, lakini unapokosa uaminifu, watu wanasahau kabisa kama huwa unafanya kazi nzuri.

Unapokuwa mwongo na usiyetimiza ahadi zako, watu watakachofikiria cha kwanza wanapokutana na wewe ni hicho. Huyu mtu anafanya kazi sawa, lakini hatabiriki, huwezi kumtegemea.

Vitu hivi vidogo vinawazuia watu wengi kuweza kupiga hatua, lakini cha kushangaza ni kwamba wengi hawana hata habari juu ya hilo. Hii ni kwa sababu wanakuwa wanaendesha maisha yao kwa mazoea, wakifikiri kile wanachoamini wao ndiyo wanaamini wengine.

Weka juhudi kubwa, pambana mno, lakini kumbuka vitu vidogo vidogo ambavyo vinaweza kuwa kikwazo kwako. Chunguza kila tabia uliyonayo kwenye shughuli zako, na ona ni kwa namna gani inaweza kupelekea kupunguza thamani ya juhudi kubwa unazoweka.

SOMA; UKURASA WA 348; Vitu Vidogo Vinavyoweza Kuharibu Siku Yako….

Mara nyingi vitu vidogo ambavyo huvioni na unafanya kwa mazoea, vinakuwa na madhara makubwa kwenye thamani ya juhudi kubwa unazoweka.

Hili pia linakwenda kwenye mahusiano yetu na wengine. Tunaweza kuwa tunakazana kuweka juhudi kujenga mahusiano yetu, lakini tabia zetu ndogo ndogo zikawa zinayaharibu mahusiano tunayokazana kujenga.

Kuwa makini na kila unachofanya au kutokufanya, kinaweza kuharibu juhudi kubwa unazokazana kuweka kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.