UKURASA WA 976; Huwezi Kumdanganya Mtu Yeyote Hapa Duniani Ila Wewe…

By | September 2, 2017

Kuna watu ambao ni waongo, kuanzia kwenye maneno, matendo na hata aina ya maisha wanayoishi. Watu hawa huwa wanapenda kuonekana tofauti na walivyo, ili kupata chochote wanachotaka kukipata.

Japokuwa uongo unaweza kuwasaidia kwa wakati mfupi, baadaye huwa na madhara makubwa zaidi kuliko faida walizopata.

Na hasara kubwa zaidi ya uongo siyo kwa wale ambao wanadanganya, bali kwa yule ambaye anadanganya. Yaani yule anayedanganya, anaumizwa zaidi na uongo wake kuliko hata wale ambao wanadanganywa.

IMG-20170720-WA0004

Kwa mfano, unapomdanganya mtu kitu ambacho hajui, anaweza kukuamini, ukapata unachotaka. Uliyemdanganya ataondoka akiwa na amani kwa sababu anajua ulichomwambia ndiyo ukweli. Lakini wewe utabaki ukijisuta kwenye nafsi yako kwamba umedanganya. Sasa hapo wewe unaumia zaidi kuliko yule uliyemdanganya.

Hata kama yule uliyemdanganya atagundua wewe ni mwongo, akishaondoka anasahau kuhusu wewe, anaendelea na maisha yake na changamoto zake. Lakini wewe utaendelea kubaki na kumbukumbu za uongo wako na jinsi ulivyokuumbua.

Hapo bado kuna kutunga uongo ili kuziba uongo. Uongo wowote huwa haujitoshelezi, kuna wakati utahitaji uongo zaidi ili kufunika uongo wa kwanza, huu ni utumwa wa hali ya juu mno.

Kuna utani kwamba ukiwa mwongo basi uwe na kumbukumbu, na huu siyo tu utani bali ni uhalisia. Kwa sababu unachodanganya siyo halisi, na unadanganya mara nyingi, kuna wakati utasahau ulimwambiaje mtu. Hali hiyo inakufanya uteseke sana kabla hujafanya lolote, kujihakikishia kwamba hujawahi kusema kitu cha tofauti na unachokwenda kufanya.

SOMA; UKURASA WA 915; Hivi Ndivyo Unavyotengeneza Siku Mbaya Kwako…

Yote hayo ni mateso makubwa, lakini bado watu wanaendelea kudanganya.

Ukweli ni uhuru, ukweli hauhitaji kutetewa na wala ukweli hauhitaji uwe na kumbukumbu kubwa. Ukweli unabaki kuwa ukweli, haubadilishwi na chochote. Hivyo inakulipa zaidi iwapo utakuwa mkweli wakati wote, itakujengea uaminifu na kukupunguzia changamoto.

Katika hali ya uongo, anayedanganya anadhurika zaidi kuliko anayedanganywa. Hivyo usidanganye, na ikitokea mtu amekudanganya, mcheke kwa kujua yeye anajiharibia zaidi kuliko wewe uliyedanganywa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.