UKURASA WA 980; Uongo Unaingilia Masikioni, Na Kutokea Machoni…

By | September 6, 2017

Upo usemi maarufu kwamba kusoma huwezi, je picha nayo huoni? Tunaweza kuuboresha usemi huu na ukawa kusikia husikii, je hata kuona nako shida.

Iko hivi rafiki, uongo wowote huanzia kwenye kusikia. Yaani watu watakuambia mambo mengi ambayo ni uongo. Unaweza kusikiliza na ukaamini kabisa unachoambiwa ndiyo kilivyo au ndiyo uhalisia.

Lakini unapopata nafasi ya kuona kwa macho yako mwenyewe, kama upo makini, utaona ukweli. Kama unaangalia kwa umakini, ukiwa na udadisi, utaona ni wapi mambo hayaendani.

Na kama anayekueleza unamwona, utaona hata mashaka ambayo anayekuambia ukweli anakuwa nayo. Au kama utamuuliza swali, utaona namna anababaika kujibu swali lako.

IMG-20170720-WA0005

Hivyo rafiki, angalia sana kile ambacho unaambiwa, kama ni mtu anakuambia kitu, mwangalie vizuri na kwa undani. Kama ni kitu unaoneshwa, hata kama unaambiwa uharakishe, angalia vizuri na kwa umakini. Uongo ni vigumu sana kuyalaghai macho.

SOMA; Uongo Huu Unaojiambia Kila Siku, Ni Adui Mkubwa Wa Mafanikio Yako.

Kwa upande wa pili, kama unaambiwa kitu chochote ambacho hujakiona, kipe nafasi ya uongo au hata kuongezwa chumvi. Kwa maana nyingine, chochote unachoambiwa, usikipokee kwa asilimia 100 kama ndiyo ukweli. Jua kuna vitu huenda hujaambiwa na vingine huenda vimekuzwa kuliko uhalisia wake. Hii ni kwa matumizi yako mwenyewe na siyo lazima umwambie mtu sikuamini kwa sababu sijaona. Badala yake fanya maamuzi yako ukijua kuna vitu ukweli wake huna uhakika nao.

Yatengeneze macho yako kuona kile ambacho unapaswa kuona na siyo kile ambacho unataka kuona. Macho yana nguvu kubwa ya kugundua uongo ulipo yatumie vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.