UKURASA WA 985; Njia Pekee Ya Kwenda Salama Hapa Duniani…

By | September 11, 2017

Maisha ya mafanikio yana changamoto nyingi, changamoto za ndani ya mtu mwenyewe na changamoto za nje.

Changamoto za nje ni kama kukosolewa, kupingwa, kusemwa vibaya na hata kudhulumiwa na wengine. Unapoanza kuweka juhudi ili kutoka hapo ulipo, utawavuruga wengi na hawatafurahia hilo. Hivyo watafanya kila jitihada kuhakikisha unabaki pale ulipo sasa. Na hapo ndipo vinaibuka vitu kama hivyo vya kukukatisha tamaa ili urudi pale ulipo.

IMG-20170611-WA0001

Changamoto za ndani ni kama kukata tamaa, kukosa uvumilivu, kuchoka, kutaka kushindana na wengine na mbaya zaidi, kiburi cha mafanikio. Haya ni mambo ambayo yanakuwa ndani yako, labda umejaribu sana hupati unachotaka, unaanza kukata tamaa, au kitu kinachukua muda sana na unakosa uvumilivu. Wakati mwingine unajikuta unawaangalia wengine na kuona wao wako vizuri kuliko wewe na kutaka kuwaiga au kushindana nao. Na kuna sumu mbaya ya kiburi cha mafanikio, baada ya kuanza kupata mafanikio unaona wewe ndiye unayejua kila kitu, hakuna anayejua kama wewe.

Changamoto zote hizi zinafanya maisha ya mafanikio kuwa magumu na wakati mwingine ya ukwepe mkubwa. Na hapa ndipo tunapohitaji kitu muhimu kinachoweza kutuvusha kwenye aina hii ya maisha.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Upacha wa dunia na jinsi ya kuutumia kuwa na maisha bora.FALSAFA MPYA YA MAISHA; Upacha wa dunia na jinsi ya kuutumia kuwa na maisha bora.

Kitu pekee cha kutuvusha ni upendo. Upendo una nguvu kubwa ya kutufanya tuendelee kuweka juhudi. Upendo unatuwezesha kuendelea kushirikiana na wengine. Na upendo unatupa nguvu ya kuendelea hata pale mambo yanapoonekana magumu.

Upendo tunaozungumzia hapa ni mpana, ni upendo wa kila aina.

Unaanza na upendo kwako wewe binafsi, lazima ujipende sana wewe mwenyewe, uamini kwenye ndoto zako na uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Lazima uwapende wale wanaokuzunguka, ukianza na wale ambao ni wa muhimu sana kwako. Hawa wanaweza kuwa sababu ya wewe kuweka juhudi zaidi kwenye kile unachofanya. Lazima pia uwapende watu wengine wote, licha ya changamoto walizonazo.

Upendo pia unahusika kwenye kile unachochagua kufanya. Kwa sababu kila kitu kina changamoto, unapopenda unachofanya, changamoto hazitakukwamisha. Badala yake utaendelea kuweka juhudi kubwa. Na pia hutapata muda wa kujilinganisha na wengine, kushindana au kutaka kuwaiga.

Upendo una nguvu kubwa ya kutuvusha kwenye changamoto tunazopitia na kutufikisha kwenye mafanikio makubwa. Hili ni eneo muhimu tunalopaswa kulifanyia kazi kila siku kwenye maisha yetu, kwa ajili ya mafanikio yetu.

Na hata hivyo, mafanikio yetu siyo kwa ajili yetu wenyewe, ni kwa ajili ya wengine pia, hivyo kama hatutakuwa na upendo kwao, mafanikio yetu yatakuwa ya mashaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.