BIASHARA LEO; Siyo Lazima Kila Wakati Uuze…

By | September 12, 2017

Wapo wafanyabiashara ambao wana mtazamo kwamba kila wakati lazima wauze. Hivyo anapokuwa mteja ambaye anauhitaji wa kitu ambacho wao hawana, huhakikisha wanampatia kitu kingine ili tu asiondoke bila ya kununua.

Hii ni mbinu nzuri ya kuwasaidia wateja hasa kama kile unachowapa kitawasaidia kweli. Lakini kama hakitawasaidia, na wewe utakuwa umesukumwa na kuuza tu, utapoteza wateja.

Kuwa tayari kuwaambia wateja ukweli hata kama utapelekea wewe kutokuwauzia. Kwa sababu wakati mwingine wafanyabiashara huficha ukweli wakiamini kuwapa wateja ukweli kutawapelekea wasinunue.

Biashara

Kama kuna mgongano kati ya ukweli na kuuza, yaani kama ukisema ukweli basi mteja hatanunua, mara zote sema ukweli. Kuficha ukweli hata kama ni mdogo kiasi gani kwa lengo tu la kuuza, mara zote huleta madhara zaidi kwenye biashara yako.

Usitake kuuza kila mara kwa kutumia kila njia, mpe mteja ukweli kwa namna ulivyo, halafu yeye afanye maamuzi iwapo atanunua au la.

SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuwa Mwaminifu Kwenye Ulimwengu Wa Sasa Uliojaa Kila Aina Ya Hila.

Ukimwambia mteja ukweli leo na asinunue, atajenga imani kwako na siku nyingine atakuja tena. Ukimficha mteja ukweli na akanunua, atakuja kuujua ukweli na hatokuja kununua kwako tena.

Hivyo ni muhimu kusema ukweli mara zote, hata kama utapelekea mteja kutonunua, wapo wengine watanunua na huyo atakuja kununua wakati mwingine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.