UKURASA WA 986; Njia Ya Akili Kutafuta Urahisi Wa Maisha…

By | September 12, 2017

Kuna mambo mengi mno yanayoendelea kwenye mazingira yanayokuzunguka, kiasi kwamba kama akili yako ingekuwa inayachakata yote na kukuletea kila kitu kwenye mawazo, ungeweza hata kuchanganyikiwa.

Hii ni kwa sababu mambo ni mengi mno, hivyo akili zetu zimejifunza kuyapokea mengi na kuyafanyia kazi bila ya uelewa wetu wa moja kwa moja.

Kwa mfano, ukiingia kwenye chumba ambacho kina saa ya ukutani ya mshale, utakuwa unasikia ule mshale ukizunguka kwa sauti, lakini baada ya muda husikii tena ile sauti. Siyo kwamba imeondoka, bali akili imeshajua siyo sauti hatari na hivyo huna haja ya kusumbuka nayo.

Eneo

Kadhalika kama umewahi kuenda eneo lenye harufu ya tofauti, unapofika kwa mara ya kwanza utasikia harufu ni ya tofauti. Lakini kadiri unavyokaa pale, ile harufu huisikii tena. Siyo kwa sababu harufu imeondoka, bali kwa sababu akili yako imeona harufu hiyo haina hatari, na kuamua kuipotezea.

Hii inatuonesha ni kwa namna gani akili zetu zinaweza kututenga na mambo mazuri na makubwa kwa mafanikio yetu. Fursa zipo nyingi sana zinatuzunguka, lakini akili zetu zinapuuza yale mambo ambayo hatujisumbui nayo.

Mfano mwingine, leo ukiwa barabarani, sema magari mekundu ni mengi kweli. Utashangaa kila unapokatiza unakutana na gari nyekundu. Siyo kwamba yameongezeka leo, bali ulikuwa unayapotezea, kwa sababu mawazo yako hayakuwa kwenye magari hayo mekundu.

SOMA; UKURASA WA 953; Unachokichukia, Unakipa Nguvu Ya Kuendelea Kukusumbua…

Hivyo tunaweza kusema kwamba tunachoona siyo uhalisia, bali ni kile ambacho sisi tumechagua na tunataka kuona.

Na muhimu sana ni kwamba, zile ndoto zetu, yale maono makubwa ambayo tunayo, tunapaswa kuhakikisha hayaondoki kwenye mawazo yetu kabisa. Kwa sababu kwa kufanya hivyo, tunazifundisha akili zetu kwamba siyo muhimu na inaweza kupotezea.

Hii ndiyo sababu watu wengi huwa na malengo makubwa mwanzo wa mwaka, lakini baadaye wanayasahau kabisa. Kwa sababu hawayasisitizi kwenye akili zao, akili zinaona siyo muhimu na kupuuza.

Muhimu sana uandike maono na malengo yako kila siku. Lazima uwe unayafikiria kwa muda mwingi wa siku yako. Na hapo akili yako itaendelea kuyaangalia mazingira na kukuletea zile fursa ambazo zitakuwezesha kufanyia kazi malengo yako.

Lazima tujifunze na tuweze kutumia akili zetu vizuri, la sivyo akili zitatutumia na tukiruhusu zitutumie, hatutaweza kufanya makubwa, kwa sababu kwa asili, akili zetu hutafuta urahisi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.