UKURASA WA 1001; Utakutana Na Bahati…

By | September 27, 2017

Kwenye maisha huenda umewahi kuona mambo yametokea kwa watu na kusema watu hao wana bahati kweli. Labda wanakuwa wamekutana na kitu ambacho kimerahisisha zaidi safari yao ya mafanikio.

Wakati mwingine ni wewe unakuwa umekutana na hali fulani na kujiona mwenye bahati, au wengine wakasema una bahati sana.

Swali ni je bahati imekudondokea tu wewe au mwingine bila ya kuwepo chochote ambacho kimechochea bahati hiyo?

Kwa sehemu kubwa jibu ni hapana, bahati ile haiwi imetokea tu hewani, bali ni matokeo ya hatua ambazo mtu unakuwa umechukua. Maandalizi ambayo unakuwa umefanya na hatua ambazo unakuwa umechukua zinakuweka kwenye nafasi ambayo jambo lolote linapotokea, inakuwa rahisi kwako kulitumia kwa manufaa yako. Na hiyo ndiyo bahati.

Ni vigumu sana bahati kwenda kwa kila mtu au kwenda kwa yeyote. Na inapotokea bahati hiyo imeenda kwa yeyote ambaye hakuwa amejiweka kwenye mazingira ya kuweza kuitumia, haiwi tena bahati kwake.

Ninachotaka kukuambia rafiki yangu ni kwamba kila mtu anaweza kukutana na bahati kama atakaa kwa muda mrefu kwenye kile anachofanya. Kama kila wakati ataendelea kuwa bora zaidi akiweka juhudi kwenye kile anachofanya. Kwa hatua za aina hiyo, fursa yoyote inayojitokeza, inampa nafasi kubwa yeye kuliko ambaye hajakaa muda mrefu na hana maandalizi.

SOMA; UKURASA WA 10; Umetengeneza Ulimwengu Wako Mwenyewe.

Wanasema bahati ni pale fursa inapokutana na maandalizi. Fursa zipo nyingi, changamoto kubwa ni watu kukosa maandalizi. Watu wengi wamekuwa wakitaka mambo yatokee haraka, hawana uvumilivu wa kuweka juhudi kwa muda ili kutengeneza bahati zao. wengi huacha na kukata tamaa haraka, kabla hata hawajawa na maandalizi ya kuwatosha kukutana na bahati.

Kama unataka kukutana na bahati, chagua kile ambacho unataka kufanya, weka juhudi zako zote kwenye kitu hicho, jipe muda wa kukifanya kwa kutokutegemea matokeo ya haraka, na kila siku weka juhudi ili kuwa bora zaidi kwenye hicho unachofanya. Kwa njia hiyo, lazima utakutana na bahati, na wasioelewa watasema una bahati kuliko wao. Kumbe hata wao wangeweza kutengeneza bahati hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.