UKURASA WA 1002; Kujua Kila Kitu Na Kujifunza Kila Kitu…

By | September 28, 2017

Nimekuwa natumia muda mwingi kusoma na kujifunza falsafa mbalimbali ambazo zimekuwepo duniani. Na kitu kimoja ambacho najifunza ni kwamba, karibu kila falsafa tunayoijua ina msingi wake kwenye mafundisho ya mwanafalsafa Socrates.

Kila msingi wa falsafa, una ufanano na misingi ya kifalsafa iliyoasisiwa na Socrates. Na hata misingi mingi ya kidini, ukiiangalia kwa undani, unagundua ina mizizi yake kwenye falsafa za Socrates.

Lakini ukimwangalia huyu Socrates kuna jambo moja la kushangaza sana, hakuwahi kuandika kitabu, wala kutoa mafunzo ya kifalsafa. Kitu kikubwa alichokuwa akifanya ni kuhoji na kuwataka watu wafikiri zaidi ya kuenda kwa mazoea.

Socrates alisifika kwa kuwakusanya watu na kuendesha mahojiano na mijadala iliyopelekea mtu kufikiri zaidi na kutafuta ukweli wa jambo lolote lile.

Socrates alikiri kwamba kuna kitu kimoja ambacho anajua kwenye maisha yake, na kitu hicho ni kwamba hakuna anachojua. Hivyo kama Socrates hakuwa anajua, ilimlazimu yeye kujifunza kila wakati.

Tunaishi kwenye dunia ambayo kila mtu anajua kila kitu. Kila mtu ni mshauri, kila mtu ni mkosoaji, na kila mtu ana la kusema kuhusu kila jambo. Ni vigumu kukutana na mtu ambaye anasema hajui kwenye zama hizi. Kila mtu anajua na ndiyo sababu watu hawaoni umuhimu wa kujifunza.

Kama tunataka kupiga hatua, kama tunataka kujua zaidi ya kile kidogo ambacho tunajua, basi tunapaswa kubadili mtazamo wetu, tutoke kwenye mtazamo kwamba tunajua kila kitu na tuende kwenye mtazamo kwamba tunajifunza kila kitu.

SOMA; UKURASA WA 215; Kufanikiwa, Jua Kitu Ambacho Wengine Hawajui, Ila Usiwe Mchoyo.

Hata kama kipo kitu una uhakika nacho kabisa, kuwa tayari kujifunza tena, jifunze kutoka kwa wengine, jifunze kutokana na makosa yako na ya wengine, jifunze kutokana na tafiti na jifunze kwa wale waliokutangulia.

Jifunze kila kitu ni mtazamo mzuri kuliko kujua kila kitu, na hii itakuwezesha kujua zaidi na hata kujenga busara za maisha ambazo zitakusaidia sana.

Usijione unajua kila kitu, bali jipange kujifunza kila kitu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.