MWONGO WA KUFIKIA UBILIONEA (2020 – 2030).

By | April 11, 2022

MWONGO WA KUFIKIA UBILIONEA (2020 – 2030).

Muongo wa 2020 – 2030 ni muongo wa kufikia kiwango cha utajiri cha UBILIONEA kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Hiki ni kipindi ambacho kila mwanachama anapaswa kufikia uhuru wa kifedha kwenye maisha yake.

Ni kupitia uhuru huo wa kifedha ndipo kila mwanachama anaweza kuwa huru na maisha yake.

Katika kujenga uhuru huu wa kifedha na kufikia ubilionea, njia kubwa tatu zinatumika.

👉Njia ya kwanza ni biashara.

Kila mwanachama anajenga biashara zinazojiendesha zenyewe bila ya kutegemea uwepo wake moja kwa moja.

Biashara ndiyo njia kuu ya kutengeneza mzunguko wa fedha (cashflow).

👉Njia ya pili ni uwekezaji kwenye masoko ya mitaji (paper assets).

Kila mwanachama anafanya uwekezaji kwenye masoko ya mitaji ili kuweza kutunza fedha kwa namna ambayo haipotezi thamani.

Kwenye masoko ya mitaji ni rahisi kuipata fedha pale unapokuwa na uhaitaji nayo, lakini pia uwekezaji unaokuwa umefanya unakua thamani kadiri muda unavyokwenda, tofauti na kuweka tu fedha benki.

Kwenye uwekezaji wa masoko ya mitaji kuna maeneo matatu ambayo kila mwanachama anapaswa kuyafanyia kazi.

✔Uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja. Hapa njia kuu ni kupitia UTT AMIS ambayo ina mifuko mitano ya uwekezaji.

✔Uwekezaji kwenye hisa. Hapa unanunua hisa kwenye makampuni yaliyoorodheshwa kwenye soko la hisa.

✔Kununua hatifungani (bonds). Hapa unanunua hatifungani ambao ni uwekezaji salama zaidi na wenye malipo ya uhakika, japo siyo makubwa sana.

👉Njia ya tatu ni uwekezaji kwenye mali (real estate).

Mali ndiyo njia ya kutunza utajiri mkubwa ambao mtu anautengeneza.

Kwenye uwekezaji huu kuna maeneo matatu ya kufanyia kazi;

✔Kuwa na majengo ya kupangisha na kuuza.

✔Kuwa na ardhi, viwanja na mashamba.

✔Kufanya kilimo cha muda mrefu kama kilimo cha miti.

Mkakati mkuu ni kutengeneza fedha kupitia biashara kisha kuziwekeza kwenye masoko ya mitaji na mali.

⭐MKAKATI WA BIASHARA.

Biashara ndiyo nyenzo kuu ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha kwenye huu muongo.

Ndiyo njia rahisi na ya uhakika ya kufika kwenye ubilionea kwenye kipindi tulichonacho.

Katika kuhakikisha kila mwanachama anatumia biashara kufika kwenye ubilionea, mkakati ufuatao utafanyiwa kazi na kila mwanachama.

Kwenye huu muongo tutapanda ngazi tano za ujasiriamali mpaka kufika juu kabisa.

👉Ngazi ya kwanza; Kujiajiri.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2021/2022; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa kwenye angalau ngazi ya kwanza ya ujasiriamali, yaani kujiajiri.

Hata kama umeajiriwa, unapaswa kuwa na biashara ya pembeni yenye wateja ambao unawahudumia wewe mwenyewe moja kwa moja.

Kwenye ngazi hii kila mwanachama anapaswa kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki katika kuendesha biashara yake.

Mfumo unaopendekezwa zaidi ni wa THL Accounting.

👉Ngazi ya pili; Umeneja.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2022/2023; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa kwenye angalau ngazi ya pili ya ujasirimali, yaani kuwa na biashara yenye wasaidizi, hata kama bado inamtegemea kwa kila kitu.

Idadi yoyote ya wafanyakazi ni sawa, muhimu ni usiwe unafanya mwenyewe kila kitu. Na hii ndiyo hatua ya kuandaa na kuanza kutumia mfumo wa biashara.

Kwenye ngazi hii kila mwanachama anapaswa kuandaa mfumo wa kuiendesha biashara yake. Mfumo utakuwa umeandikwa vizuri na unaogusa kila eneo la biashara na ndiyo utakaofuatwa katika kuendesha biashara nzima.

👉Ngazi ya tatu; Uongozi.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2023/2024 na 2024/2025; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa kwenye angalau ngazi ya tatu ya ujasiriamali, yaani ana biashara inayojiendesha yenyewe bila ya kutegemea uwepo wake moja kwa moja. Hii ndiyo hatua ya kuanza kupata uhuru wa muda na fedha.

Ngazi hii tunaipa miaka miwili kwa sababu ina kazi kubwa ya kufanya ndani yake. Lakini katika kukamilisha miaka hiyo miwili, hakuna anayepaswa kuwa anategemewa na biashara moja kwa moja.

Kwenye ngazi hii mwanachama anausimamia zaidi mfumo kuliko kuwasimamia watu. Yeye anasimamia mfumo na mfumo ndiyo unasimamia watu. Hapa pia anaendelea kuboresha mfumo kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

👉Ngazi ya nne ; Uwekezaji.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2025/2026 na 2026/2027; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa kwenye angalau ngazi ya nne ya ujasiriamali, yaani kununua, kujenga na kuuza biashara mbalimbali au kuwa na biashara zaidi ya moja zinazojiendesha zenyewe na kuweza kuziuza.

Kwenye hatua hii ongezeko la kipato linakuwa kubwa huku uhuru ukizidi kuongezeka. Ngazi hii pia ina miaka miwili kwa sababu ina kazi kubwa ya kufanya.

Kwenye ngazi hii mwanachama anakuwa na timu ya wasaidizi wake wa uhakika (mameneja) ambao anawaweka kwenye biashara anazonunua ili waziboreshe kisha ziweze kuuzwa.

Ngazi ya tano; Ujasiriamali.

Kwenye mwaka wa mafanikio 2027/2028 mpaka 2029/2030; kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anapaswa kuwa amefikia ngazi ya tano ya ujasiriamali ambayo ndiyo ujasiriamali kamili.

Katika ngazi hii kila mmoja anakuwa ameweza kufikisha kampuni kwenye soko la hisa au kuuza leseni kwa wengine kuendesha na wakamlipa.

Hatua hii ina miaka mitatu kwa sababu ina mchakato mkubwa wa kisheria wa kufuata ili kuikamilisha.

Kwenye hatua hii, mwanachama anatengeneza fedha bila ya kufanya chochote au kuwekeza zaidi kwenye biashara.

Kazi kubwa aliyofanya huko nyuma ndiyo inakuwa inamlipa.

Kwa mkakati huu, tunapokwenda kufika mwaka 2030 kila mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA anakuwa amefikia ubilionea ambao unampa uhuru kamili wa fedha, muda na maisha na kuendelea kufanyia kazi ndoto zake nyingine alizonazo.

⭐INJINI KUU YA BIASHARA.

Katika kufanyia kazi mkakati wa biashara, kuna injini kuu ya biashara ambayo ndiyo inapaswa kufanyiwa kazi.

Injini hiyo ina pande mbili.

👉Upande wa kwanza ni namba muhimu za biashara zinazopimwa.

Namba hizo ni;

 1. Mtaji unaozunguka kwenye biashara.

 2. Mauzo yanayofanyika.

 3. Idadi ya wateja ambao biashara inao.

 4. Gharama za kuendesha biashara.

 5. Faida ambayo biashara inatengeneza.

👉Upande wa pili ni maeneo muhimu ya kufanyia kazi ili kuzalisha namba muhimu zinazopimwa.

Maeneo hayo ni;

 1. Masoko, kuwafikia wateja tarajiwa na kuwafanya wajue kuhusu uwepo wa biashara.

 2. Kuwageuza wateja tarajiwa kuwa wateja kamili kwa kuwashawishi waweze kununua.

 3. Kuwafanya wateja warudi kununua mara kwa mara.

 4. Kuwashawishi wateja kufanya manunuzi zaidi ya walivyokuwa wamepanga.

 5. Kuongeza kiwango cha faida kwenye mauzo yanayofanyika.

 6. Kudhibiti mzunguko wa fedha kwenye biashara.

Injini hii ya biashara inapofanyiwa kazi vizuri, ukuaji wa biashara unakuwa ni wa uhakika.

⭐MKAKATI WA UWEKEZAJI.

Uwekezaji ndiyo njia ya kutunza utajiri ambao mtu ameujenga.

Ili kujenga na kutunza utajiri wa ngazi ya ubilionea kwenye KISIMA CHA MAARIFA, mkakati ufuatao utafanyiwa kazi.

👉Kila mwanachama atakuwa na akaunti maalumu ya uwekezaji ambapo ndipo atakuwa anaweka fedha anazopanga kuwekeza.

👉Faida inayopatikana kwenye biashara, nusu inakwenda kwenye akaunti ya uwekezaji na nusu inarudi kukuza mtaji wa biashara.

👉Mwaka wa mafanikio 2021/2022 kila mwanachama anapaswa kuwa na akaunti ya uwekezaji UTT na kuwa ameanza kufanya uwekezaji huko.

👉Mwaka wa mafanikio 2022/2023 kila mwanachama anapaswa kuwa na uwekezaji kwenye hisa na hatifungani.

👉Mwaka wa mafanikio 2023/2024 na 2024/2025 ni mwaka wa kuwa na uwekezaji kwenye ardhi na kilimo cha muda mrefu.

👉Mwaka wa mafanikio 2025/2026 mpaka 2029/2030 ni mwaka wa kufanya uwekezaji mkubwa kwenye majengo.

Pia uwekezaji endelevu kwenye maeneo mengine utakuwa unafanyika.

Kwenye eneo la uwekezaji, mtu anaweza kuwahi kadiri awezavyo au inavyoruhusu kwa upande wake.

Muhimu ni katika kila kipindi cha mwaka wa mafanikio mtu awe na uwekezaji kwenye maeneo tuliyoyachagua.

⭐SIFA YA KUPATA NAFASI YA KUENDELEA KUWA KWENYE KISIMA CHA MAARIFA.

Katika kupima sifa za wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, madaraja A, B, C, D, E na F yanatumika.

Daraja linatokana na vitu vitano muhimu vinavyopimwa kwa kila mwanachama.

Vitu hivyo ni kama ifuatavyo;

 1. Kulipa ada kwa wakati.

 2. Kuiishi misingi ya KISIMA CHA MAARIFA.

 3. Kutuma tathmini za wiki, mwezi na robo mwaka.

 4. Kuwa kwenye klabu za KISIMA CHA MAARIFA na kushiriki kwa ukamilifu.

 5. Kushiriki semina za kukutana ana kwa ana za mwaka za KISIMA CHA MAARIFA.

Madaraja yanapatikana kama ifuatavyo;

A – 5/5 (Anafanya yote matano).

B – 4/5 (Anafanya manne kati ya matano).

C – 3/5 (Anafanya matatu kati ya matano).

D – 2/5 (Anafanya mawili kati ya matano).

E – 1/5 (Anafanya moja kati ya matano).

F – 0/5 (Hafanyi lolote katika hayo matano).

Sifa ya kuendelea kupata nafasi kwenye KISIMA CHA MAARIFA ni kuwa daraja A au B.

Daraja C anaweza kupata nafasi, kama ataahidi na kutekeleza kupanda daraja.

CHINI YA DARAJA C HAKUNA NAFASI KWENYE KISIMA CHA MAARIFA.

⭐VITABU VYA MWONGOZO.

Katika muongo huu wa kuelekea kwenye ubilionea, kuna vitabu vitano vya mwongozo ambavyo tunavisoma/kuvisililiza na kuvifuata kama vilivyo bila ya kubadili chochote.

👉Billionaire In Training cha Bradley Sugars.

Hiki ndiyo kitabu kikuu tunachokifuata kama mwongozo kwenye kujenga biashara.

👉Instant Millionaire cha Mark Fisher.

Hiki ni kitabu cha kujijengea fikra sahihi za kufika kwenye ubilionea.

Tukijua fikra ni kitu chenye nguvu kubwa kwenye maisha yetu.

Hivyo kwa kuzitumia vizuri fikra zetu, tuna uhakika wa kupata kile tunachotaka.

👉How to be a billionaire cha Martin Fridson.

Hiki kinatupa uzoefu kutoka kwa mabilionea waliotutangulia, jinsi walivyoweza kufika kwenye ubilionea.

👉Mwongozo wa maisha ya mafanikio cha Kocha Dr Makirita Amani.

Hiki ndiyo mwongozo mkuu wa kuyaishi maisha yetu ya kila siku kwa namna ambayo itatuwezesha kupata kile tunachotaka.

👉Your First 100 Million cha Dan Pena.

Hiki kinatupa fikra za kimapinduzi (quantum leap) katika kufikia lengo la ubilionea.

Kinatupa mbinu zote za kuanzisha, kukuza na kuuza biashara.

⭐MAMBO MATATU YA KILA MTU KUJENGA.

Kuna mambo matatu muhimu ambayo kila mwanachama anapaswa kuyajenga ili safari hii ya kuelekea kwenye ubilionea iwezekane kwake.

👉Moja ni kulijua KUSUDI LA MAISHA.

Hapa lazima ujue uko hapa duniani kufanya nini.

Kusudi ndiyo linakupa nguvu ya kuendelea kupambana bila kuchoka.

👉Mbili ni kuwa na NDOTO KUBWA.

Ubilionea ni matokeo, ambayo yanahitaji mchakato ndiyo yapatikane.

Mchakato wako wa kufika kwenye ubilionea ni ndoto kubwa ulizonazo.

Unapaswa kuwa na ndoto kubwa unazoziona kwa macho na unazopambana kuzifikia.

Amini sana kwenye ndoto hizo na kuwa na uhakika wa kuzifikia.

Amua utazifikia ndoto hizo au utakufa ukiwa unazipambania, hakuna namna nyingine.

👉Tatu ni kuwa na MTU WA MFANO (ROLE MODEL).

Unapaswa kuchagua mtu au watu wa mfano kwako.

Watu ambao unavutiwa sana na maisha waliyoishi na mafanikio waliyofikia.

Watu hao wanakupa sababu na imani ya wewe kupambana ili kufanikiwa.

Wanaweza kuwa hai au wamekufa.

Muhimu sana ni ukishachagua mtu/watu hao basi unapaswa kujifunza kila kitu kuwahusu wao.

Kadiri unavyowajua watu hao ndiyo inakuwa rahisi kuwatumia kama kielelezo cha wewe kufika unakotaka.

Mwongozo huu umeandaliwa na;

Muuza Matumaini Kocha Dr. Makirita Amani.

Mkuu wa jeshi la KISIMA CHA MAARIFA.

Bilionea Mafunzoni.

Raisi wa Tanzania katika maandalizi.

MWONGO WA KUFIKIA UBILIONEA (2020 – 2030).

Category: KUTOKA KWA KOCHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.