UKURASA WA 917; Tumia Njia Hii Kujijengea Nidhamu Binafsi…

By | July 5, 2017

Nidhamu binafsi ndiyo msingi mkuu wa mafanikio kwenye kila eneo la maisha yetu. Iwe ni kwenye afya, mahusiano, fedha, kazi na hata biashara. Bila nidhamu binafsi, huwezi kufika viwango vya juu vya mafanikio, kwa sababu changamoto ni nyingi na hata usumbufu pia ni mwingi.

Watu wote waliofanikiwa, wana nidhamu binafsi ya hali ya juu. Wanapanga kufanya jambo na wanalifanya kweli. Hawana kuahirisha na wala hawajidanganyi kesho ndiyo muda mzuri zaidi wa kufanya. Wanafanya leo na kwa wakati waliopanga kufanya, iwe wanajisikia kufanya au la.

Uzuri ni kwamba, hakuna anayezaliwa akiwa na nidhamu binafsi, hizi ni tabia ambazo tunajifunza hapa duniani. Hii ina maana kwamba, hata wewe hapo ulipo, unaweza kujijengea nidhamu binafsi na kuweza kufanya yale makubwa unayotaka kufanya.

Kikwazo kikubwa cha kujijengea nidhamu binafsi, ni tabia yetu ya kutafuta urahisi pale tunapokutana na ugumu. Kupanga tunapanga vizuri sana, na hata kuanza tunajitahidi kuanza, lakini tunapokutana na ugumu, hatuendelei, badala yake tunaangalia njia rahisi ya kutorokea.

Una changamoto ya kifedha inayokukabili, badala ya kukaa chini na ufikiri kwa kina unatokaje hapo ulipo, unakimbilia kuperuzi mitandao ya kijamii, au kufuatilia habari, au kujistarehesha kwa vilevi.

Hizo ni tabia za wasiofanikiwa, unachopaswa kufanya wewe mwanamafanikio, ni kufanya kile ambacho umepanga kufanya, iwe unajisikia kufanya au la.

Unapoanza kufanya jambo, ukakutana na ugumu, usikimbilie kutafuta urahisi, badala yake kaa na ugumu ule kwa muda uliopanga kufanya jambo hilo. Kila unapojishawishi uache kwanza na kuendelea baadaye, usijisikilize, badala yake endelea kufanya.

Kila unapoweka kengele ya kukuamsha ili uamke mapema, kengele ikalia lakini ukajiambia ulale tena dakika chache, huo ndiyo wakati wa kuamka haraka sana.

Kwa kifupi, kujijengea nidhamu binafsi, jibishie wewe mwenyewe. Ukishapanga kitu, usikubali maelezo yoyote mbadala unayojipa, hata yawe mazuri kiasi gani. Wewe fanya kama ulivyopanga, hata kama hutapata matokeo uliyotarajia kupata, kitendo cha kufanya tu ni hatua nzuri kupiga.

Ukiweza kujishinda wewe mwenyewe, hakuna yeyote au chochote kitakachoweza kukushinda.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 917; Tumia Njia Hii Kujijengea Nidhamu Binafsi…

  1. Pingback: UKURASA WA 917; Tumia Njia Hii Kujijengea Nidhamu Binafsi… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.