UKURASA WA 1011; Matokeo Ya Kujiweka Wewe Mbele Ya Wengine…

By | October 7, 2017

Kwa asili sisi binadamu ni wabinafsi, na ubinafsi wetu umetuwezesha kuona hatari mbalimbali na kuendelea kuwepo mpaka sasa.

Lakini ubinafsi wetu huu unaweza kuwa kikwazo kikubwa kwenye maisha yetu kama hatutauelewa haraka na kuchukua hatua.

Kwa kawaida watu hujiangalia wao wenyewe kwanza, kwenye kila jambo, lazima mtu aangalie usalama wake mwenyewe kwanza, kabla hajaangalia wengine.

Changamoto kubwa sana ni kwamba hakuna mstari, au kama upo basi ni mwembamba sana kati ya ubinafsi mzuri na ubinafsi mbaya. Unaweza kukazana kupata kile unachotaka, ukifikiri unachofanya ni sahihi, lakini kumbe unawatenga wengine, unawanyanyasa na kuwaumiza kihisia kwa kutokujali hisia zao.

Unaweza kufanya hivyo, ukapata kile unachotaka, lakini kwa gharama kubwa, ambayo ni upweke. Hakuna mtu anayependa kuwa na mtu ambaye anajiangalia yeye tu. Mtu ambaye anajali mambo yake na kuhakikisha anayapata anavyotaka, lakini hana muda na mahitaji ya wengine.

SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuwa Mwaminifu Kwenye Ulimwengu Wa Sasa Uliojaa Kila Aina Ya Hila.

Matokeo ya kujiangalia wewe mwenyewe, ya kuweka mahitaji yako mbele na kupuuza ya wengine ni upweke. Watu watakuogopa kama ukoma, watakukimbia kwa sababu wanajua hakuna wanachonufaika nacho kutoka kwako.

Wakati mwingine hata kama unachopata ni sahihi kabisa, njia unayotumia inaweza ikawa inawatenga wengine, na kujiona kama kushirikiana na wewe kunapelekea wao kunyonywa.

Ni rahisi sana kuingia kwenye hali hii kwenye safari yako ya mafanikio, kwa sababu unaweza kuwa na hamasa kubwa ya mafanikio na kutaka kutumia kila fursa kupata kile unachotaka.

Unahitaji kuweka maslahi ya wengine mbele, kuwafikiria wengine nao wanapata nini. Hili litawafanya waone unajali na kuwa tayari kushirikiana na wewe.

Kujenga mahusiano bora na wengine ni hitaji muhimu sana kwenye mafanikio yako. Hakikisha unaweka maslahi ya wengine mbele kama unavyoweka maslahi yako, na watu wataliona hilo na kuwa tayari kushirikiana na wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

 

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.