UKURASA WA 854; Acha Kuzidisha Ugumu Wa Maisha Yako…

By | May 3, 2017

Maisha yenyewe ni magumu, lakini sisi wenyewe tumekuwa tunachagua kuyafanya kuwa magumu zaidi. Tunafanya hivi kwa namna tunavyochagua kuishi maisha yetu, na hata namna tunavyochukulia mambo yetu na mambo ya wengine.

IMG-20170228-WA0006

Kwa mfano kama mpo mnaimba kwaya, wote mnaimba kwa pamoja, utajuaje mtu ambaye haimbi vizuri? Au anakosea kuimba? Utajua hilo kama wewe utaacha kuimba na kuanza kusikiliza wengine wanaimbaje. Hapo ndiyo utajua kwa hakika nani anaimba vibaya na nani anakosea. Sasa swali muhimu zaidi, kwa kujua hilo kunakusaidia nini wewe? Ukiangalia, hakuna msaada mkubwa, na zaidi ni hasara kwa sababu umeacha kuimba na kuanza kusikiliza wengine.

Hivi ndivyo tunavyochagua kuyafanya maisha yetu wenyewe kuwa magumu, zaidi hata ya yalivyo tayari. Tunachagua kuanza kufuatilia maisha ya wengine, kujali sana kuhusu wengine, na hivyo tunayaacha maisha yetu kwa muda. Tunasahau yale ambayo ni muhimu kwetu na hivyo kuzidi kurudi nyuma.

SOMA; Kwa Nini Ufurahie Ugumu Wa Kufikia Mafanikio.

Kama utaweka maisha yako kuwa kipaumbele chako namba moja, hutapata muda wa kufuatilia maisha ya wengine, na pia hutajikuta kwenye misukosuko na ugomvi na wengine. Kwa sababu hutahusika sana na mambo ya wengine kiasi cha kuibua migogoro kwa yale utakayofanya au kusema.

Weka nguvu zako na jitihada zako kuboresha maisha yako, jali kuhusu yako, usiwe mfuatiliaji sana wa mambo ya wengine na kusahau yako. Kwa njia hii utaweza kufanya makubwa, na pia utakuwa huru sana na maisha yako. Kwa sababu yale wanayofanya wengine ni biashara zao, na siyo zako.

Hapa simaanishi usishirikiane na wengine, bali usiwe mfuatiliaji wa maisha ya wengine. Ule umbea umbea na majungu ya nani kafanya nini, nani kakosea wapi, nani angepaswa kufanya vizuri zaidi, hayana msaada wowote kwako zaidi ya kukupotezea muda na kufanya maisha yawe magumu zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.