UKURASA WA 908; Kila Mtu Anaona Kile Anachojua…

By | June 26, 2017

Ukiwa na uvimbe kwenye mwili wako,

Ukienda kwa daktari wa magonjwa ya binadamu atakuambia nikikupa dawa utapona.

Ukienda kwa daktari wa upasuaji atakuambia nikikufanyia upasuaji utapona.

Ukienda kwa mganga wa kienyeji atakuambia nikikufanyia dawa utapona.

Kati ya hao nani yupo sahihi?

Kila mtu yupo sahihi, kulingana na kile ambacho anajua yeye. Lakini mpaka kujua kipi kitakusaidia wewe hasa, ni mpaka mtu ajue kwa ndani nini hasa kinakusumbua.

Kwenye maisha huwa tunafanya makosa ya kuwaamini sana watu tunaowaona ni wataalamu au wenye mamlaka, kwa sababu ya ujuzi au uzoefu wao. Tunachukua maneno yao kama sheria, hata kama siyo sahihi, na mara nyingi huwa siyo sahihi.

Kila mtu anaona kile ambacho anajua. Hii ina maana kila mtu ana upofu mkubwa sana kwenye yale asiyoyajua.

SOMA; Kinachokuzuia Kuona Mbele… … ni kuangalia nyuma.

Kwa upande wako basi, usiwe mtu wa kuamini na kuchukua kama sheria chochote unachoambiwa juu ya lolote. Badala yake jipe muda wa kuhoji zaidi, kujifunza zaidi na kufanya utafiti zaidi.

Hasa unapokuwa na matatizo, mara nyingi unakuwa na haraka ya kutaka kuyatatua, lakini haraka hiyo imekuwa haisaidii, badala yake inazalisha matatizo zaidi.

Kabla ya kuamini kile unachoambiwa, jiulize je huo ndiyo ukweli uliopo au ndicho mtu anajua? Kwa kujiuliza hivi utakwenda mbali zaidi na kuhoji zaidi, na kwa njia hiyo utajifunza mengi.

Kwa kumalizia, ukienda kwa daktari akakuambia huu mkono inabidi tuukate hakuna namna nyingine, mwambie sawa, naenda nitarudi. Halafu pata ushauri wa madaktari wengine kwanza, huenda wapo ambao wanajua njia nyingine ambayo siyo kukata mkono.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.