UKURASA WA 934; Tofautisha Kukosa Na Kutokutaka…

By | July 22, 2017

Akili zetu zinapenda uzembe sana, kwa sababu hazitaki kusumbuka, ndiyo maana watu wengi huwa wanatafuta njia rahisi na ya mkato ya kupata chochote wanachotaka.

Unakumbuka ile hadithi ya sizitaki mbichi hizi? Kwamba sungura aliziona ndizi, akaanza kurukia, karuka mpaka kachoka, halafu mwisho akajiambia kwanza ndizi zenyewe ni mbichi, wala hata sizitaki kivile.

Unaweza kuona ni hadithi ya kitoto, lakini ina funzo kubwa sana kwenye maisha. Kwa sababu mara nyingi umekuwa unafika kwenye hatua kama hiyo na kuchukua maamuzi kama ya sungura.

Kwa mfano mara ngapi umekuwa unataka kupata kitu, unakazana sana, unakikosa, halafu baadaye unajiambia hata hivyo ulikuwa hukitaki sana, huko ni kujidanganya na kujifariji.

SOMA; Hofu Inayotokana Na Kukosa Maarifa Sahihi…

Hili lipo sana kwenye upande wa fedha, mtu anafanya kazi muda mrefu, kwenye ajira inayomlipa kidogo, au anafanya biashara ndogo, inayomhitaji sana, kila akilala anafikiria fedha na maisha yanaendaje, hapati fedha hizo halafu anajidanganya kwamba hata hivyo wenye fedha hawana raha kama yeye! Hapo ndipo unaweza kuudhihirisha uzembe wa akili yako, na kujikubali pale ulipo, hivyo kushindwa kabisa kupiga hatua.

Rafiki, umefika wakati sasa wa kuacha kujidanganya, kama kweli unataka kupiga hatua. Chagua ni nini unataka kufikia, na weka kazi kufikia, ukishindwa, jiambie wazi kwamba umeshindwa na jua sababu ni nini, na zifanyie kazi na urudie mpaka upate. Linapokuja wazo lolote la kukufanya usione uzembe wako, achana nalo mara moja, maana halitakusaidia chochote.

Kubali kwamba umekosa au umeshindwa, na jipange kuhakikisha hilo halitokei. Kujidanganya kwamba hukuwa unataka sana, ni kukumbatia uzembe ambao hautakuacha salama.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.