UKURASA WA 942; Kinachokupoteza Ni Vipaumbele…

By | July 30, 2017

Mwandishi mmoja amewahi kuandika kwamba neno kipaumbele kwa Kiingereza, zamani halikuwa na wengi, yaani lilikuwa ni priority na hakukuwa na priorities. Alisema vikishakuwa vipaumbele basi maana yake halisi inapotea. Kinapaswa kuwa kipaumbele, kitu kimoja ambacho unakipa nafasi na kuachana na vitu vingine vyote kwa wakati huo.

Nimekuwa nafikiria hilo kwa kina, na ninaona ukweli wake kila mara. Pale tunapokuwa na mambo mengi ya kufanya, hata kama yote ni muhimu, bado tunashindwa kutekeleza kitu kikubwa. Hii ni kwa sababu tunabeba mambo yote muhimu kwa wakati mmoja, tunajipa vipaumbele.

Wengi hawawezi kuchagua jambo moja pekee la kufanya kwa wakati, na kusahau mengine yote ambayo wanataka kufanya pia. Ukishashindwa kuwa na nidhamu kiasi hicho, utaishia kuhangaika kufanya mambo mengi na mwishowe hutaweza kufanikisha lolote kubwa.

Unahitaji kuchagua jambo moja la kufanya kwa wakati, jambo ambalo ndiyo muhimu zaidi, na akili yako, mwili wako, nguvu zako zote uziweke pale kwa wakati huo. Ukishakamilisha ndiyo unaweza kwenda kwenye jambo jingine kwa nidhamu hiyo hiyo.

SOMA; Kama Una Vipaumbele Huna Kipaumbele…

Usikubali kabisa kutawanya nguvu zako kwenye mambo mengi kwa wakati mmoja, utaishia kuyagusa na usione matokeo mazuri makubwa kwenye jambo lolote.

Acha kufanyia kazi vipaumbele, badala yake chagua kipaumbele kimoja, kifanyie kazi, kikiisha nenda kipaumbele kingine.

Kabla hujakamilisha kufanyia kazi kipaumbele chako, jambo jingine lolote ni usumbufu kwako. Usiruhusu kabisa likuingilie au kukuondoa kwenye kile unachofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.