UKURASA WA 862; Wanachosema Na Wanachofanya….

By | May 11, 2017

Ili kuboresha chochote unachofanya, hasa biashara basi unahitaji maoni ya watu wengine. Unahitaji maoni ya wateja wako, wale ambao wanategemea kile unachowauzia. Na pia unahitaji maoni ya wadau wengine wa karibu ili uweze kuboresha zaidi.

IMG-20170301-WA0001

Watu wamekuwa wakiomba maoni kwa watu hao muhimu, wanapata maoni na kuyafanyia kazi lakini cha kushangaza hayaleti matokeo bora. Wanafanya vile ambavyo wameshauriwa na wale wanaotegemea wanachofanya, lakini hata wale waliowashauri hawachukui hatua kwa matokeo mapya yaliyopatikana.

Watu wengi wamekuwa wakilalamika watu waliwashauri waanzishe biashara fulani na watakuwa wateja wao, wanaanzisha lakini watu wale hawaji kuwa wateja. Hii yote inasababishwa na kutokujua vizuri ni maoni gani ya kuchukua hasa kwenye biashara na kazi.

Kamwe usisikilize wanachosema watu na kufanyia kazi, badala yake angalia wanafanya nini, kisha fanyia kazi hilo. Unapowauliza watu, watakuambia kile ambacho wanajua au wanafikiri unataka kusikia. Kwa sababu watu hawapendi kuwaumiza wengine, wanajua wakikuambia ukweli wao kabisa utaumia, au kukata tamaa sana. Hivyo watakuambia kile ambacho unataka kusikia, na wewe utaona ni maoni mazuri, utafanyia kazi lakini hakuna atakayekuja katika wale waliokushauri.

SOMA; Kinachowasukuma Watu Kufanya Wanachofanya…

Hivyo acha kusikiliza na anza kuangalia. Anzisha kitu na ona watu wanakipokeaje, angalia wananunua nini zaidi, na endelea kuboresha kulingana na hatua wanazochukua. Unaweza kuwauliza lakini usichukue hatua kwa kile wanachosema, bali chukua hatua kwa kile wanachofanya. Kama wananunua kitu fulani zaidi ya kingine, hicho kinachonunuliwa sana ndiyo wanakipenda. Kama wakichukua kitu fulani wanakirudisha, basi kuna tatizo mahali. Kwa njia hii utaweza kuboresha sana biashara yako.

Kwa kuhitimisha, anza chochote na angalia watu wanakipokeaje, kisha boresha kadiri watu wanavyokipokea. Usisikilize sana maneno ya watu wanaokuambia fanya hivi au fanya vile, ni waongo ambao wanataka kukubembeleza na usiumie. Dunia haina huruma ya aina hiyo, inakulipa kadiri ya kile unachotoa. Toa kitu cha hovyo inakulipa hovyo, na toa kitu bora na inakulipa kwa ubora.

Angalia wateja wako wanafanya nini na bidhaa au huduma yako, halafu endelea kuiboresha kulingana na hatua wanazochukua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.