UKURASA WA 959; Jitangazie Uhuru Huu Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako…

By | August 16, 2017

Kila mtu ana matarajio fulani kutoka kwako, kila mtu anataka uendeshe maisha yako kutokana na anavyotaka yeye, kulingana na anavyojia na hata alivyozoea.

Lakini hebu jiulize ni watu wangapi wanaokuzunguka?

Na je iwapo utataka kutimiza matarajio ya kila mtu, utakuwa na maisha ya aina gani?

Ni dhahiri kwamba huwezi kuishi maisha bora kama utataka kutimiza matarajio ya kila mtu kwako, hivyo uhuru muhimu sana unaohitaji kujitangazia ili uweze kuwa na maisha ya mafanikio ni uhuru wa matarajio ya wengine.

Watu wote waliofanikiwa walilijua hili mapema na kujitangazia uhuru huo, hivyo kuweza kufanya makubwa bila ya kujali wengine wanasemaje juu yao.

Utakapoanza kufanya makubwa kwenye maisha yako, watu hawataacha kusema, wapo ambao watakukatisha tamaa na kukutisha, wapo ambao watakudanganya na wapo ambao watasema uongo kuhusu wewe.

SOMA;  Uhuru Pia Unatokana Na Uvumilivu Wa Wengine…

Sasa unaweza kuchagua kupambana na kila mmoja kati ya watu hao, na kuhakikisha hawakusumbui tena, au kuachana nao na kuendelea kuweka juhudi kwenye kile unachofanya.

Kuhangaika nao kunakupunguzia wewe muda na nguvu za kufanya zaidi kile unachotaka kufanya, na hivyo unakuwa umeshindwa, hata kama utakuwa umewakomesha.

Lakini unapochagua kuwapuuza wote na kukazana kwenye kile ambacho unataka kufanya, utaweza kupata matokeo mazuri sana kama unavyotegemea.

Cha kushangaza sasa, wale wale ambao walikuwa wanakukatisha tamaa na kukusema vibaya, watakuwa wa kwanza kukusifia na kusema wamekusaidia sana. Na hapa pia unaweza kuchagua kubishana nao kwamba hawajakusaidia, au ukawapuuza na kuendelea kufanya kile ambacho unafanya vizuri.

Dawa ya kila kitu ni kufanya, vitendo, hivi vina nguvu kuliko maneno yote yanayoweza kuongelewa na kila mtu.

Macho na masikio yako yawe kwenye kile unachotaka. Kwa njia hii hutaona wala kusikia wengine wanasema nini juu ya kile unachopanga kufanya, na hivyo utakuwa huru zaidi kufanya.

Wakati mwingine unaweza kufikiria labda kwa kuwasikiliza watu hao kuna kitu unaweza kujifunza au kuepuka kukosea. Kweli la kujifunza lipo, lakini kuna hatari kubwa ya kubeba hofu zao na kuacha kabisa kufanya.

Kumbuka wewe pekee ndiye mwenye ndoto kubwa ya maisha yako. Wengine hata uwaelezee vipi, bado hawataweza kukuelewa. Hivyo wataendelea kuwa na matarajio fulani kwako, wakikutaka wewe ufanye kama wanavyotaka wao.

Hapa ndipo wengi wanapopotelea na kushindwa kufanya makubwa kwenye maisha yao. Kwa kuamini watu wengine wapo sahihi kuliko wao kwenye ndoto zao.

Endelea kufanya kazi, endelea kujenga, bila ya kujali wengine wanasema nini au kutegemea nini.

Hili ni muhimu zaidi kwa wale watu wa karibu kwako, hasa wazazi na ndugu wa karibu. Wengi huamini wanakuelewa vizuri kuliko unavyojielewa wewe mwenyewe. Hivyo kutaka kukupangia namna gani uishi na nini ufanye au usifanye. Hapa ndipo pagumu sana, kwa sababu mahusiano yenu yanakufanya ushindwe kusema hapana na kusimamia kile ambacho wewe unajua ni sahihi zaidi kwako.

Na hakuna njia ya kulainisha au kukwepa hilo, ni labda uwaambie ukweli wa kile unakwenda kufanya na kufanya, au ukubaliane kwa kile wanachotaka na uishi maisha ambayo huyafurahii wala huna hamasa nayo. Sasa kwa kuwa wewe pekee ndiye utakayeyaishi maisha yako, yaani wewe ndiyo utaishi na wewe, unahitaji kufika hatua ya kufanya maamuzi muhimu kuhusu maisha yako, hata kama yanaenda kinyume na matarajio ya wengi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 959; Jitangazie Uhuru Huu Muhimu Sana Kwa Mafanikio Yako…

  1. Pingback: UKURASA WA 1099; Tofauti Ya Wabobezi Na Wachanga Kwenye Fani Mbalimbali… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.