UKURASA WA 968; Kitu Pekee Ambacho Huwezi Kufundishwa Na Yeyote…

By | August 25, 2017

Mimi ni muumini wa kujifunza, naamini mtu yeyote anaweza kujifunza au kufundishwa jambo lolote na kulielewa, iwapo ataweka juhudi za kutosha na kuwa na muda pia.

Tunaishi kwenye dunia ambayo kila kitu ambacho mtu anataka kujifunza, tayari kinapatikana. Tena tofauti na zamani ambapo ilibidi mtu akae darasani miaka na miaka, sasa hivi kwa simu yako tu unaweza kujifunza chochote utakacho.

Hata mambo makubwa sana ambayo yanahitaji uzoefu mkubwa, mtu anaweza kujifunza na kufundishwa. Mambo ambayo zamani yalionekana ni ya watu wa aina fulani pekee, sasa hivi kila mtu anaweza kufundishwa na kujifunza.

Pamoja na fursa hii nzuri ya kuweza kujifunza na kufundishwa chochote tunachotaka, kuna kitu kimoja ambacho hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kutufundisha. Na hata mtu awe na nia nzuri kiasi gani, hawezi kutufundisha.

Ni kitu ambacho lazima wewe mwenyewe ukae chini na kujifunza. Na kujifunza kwake siyo kwa ‘kugoogle’ yaani kutafuta kwenye mtandao, badala yake ni kukaa chini na kujifunza, kwa kutafakari kwa kina na kupata majibu sahihi.

SOMA; Njia Bora Kabisa Ya Kujifunza Kitu…

Huwezi kujifunza kitu hichi kupitia wengine. Na hata kama ukiwaangalia waliofanikiwa na kuiga mbinu zao, bado huwezi kujifunza kitu hicho muhimu sana kwako.

Kitu ninachozungumzia hapa ni kuhusu wewe mwenyewe. Hakuna anayeweza kukufundisha wewe kuhusu wewe.

Labda kabla sijaendelea nieleze kwamba mara nyingi wengi wanaofikiri wanajijua wao wenyewe hawapo hata karibu kwenye kujijua. Wewe siyo jina lako, wala wewe siyo kazi yako au biashara yako. Wewe siyo wajibu uliopewa kwenye jamii au familia. Wewe ni wewe, mtu pekee uliyepo hapa duniani, ukiwa na kusudi maalumu ambalo hakuna mwingine yeyote awezaye kulikamilisha.

Wewe ni wewe na hakuna anayekujua wewe kama wewe mwenyewe hujajijua. Kama hujalijua kusudi kubwa la maisha yako hapa duniani, hujajijua wewe ni nani.

Huenda wazazi na jamii ilikuambia ukiwa daktari itakuwa vizuri kwako, au mwalimu, au askari au mfanyabiashara. Hakuna ubaya wowote kwenye hayo. Ila tatizo ni moja, je unajijua wewe ni nani? Unajua upo hapa duniani kufanya nini? Unajua alama gani unapaswa kuiacha hapa duniani?

Hicho ni kitu pekee ambacho hakuna awezaye kukufundisha ila wewe. Na usije ukawalaumu wazazi au walezi wako kwa kushindwa kukufundisha hilo, kwa sababu hawajui na hivyo chochote walichokuwa wanakazana kufanya kwako, walikuwa wanajaribu tu, kuona kipi kitakufaa.

Muhimu zaidi hujapitwa na muda katika kujijua wewe mwenyewe. Wapo wanaojijua wakiwa na miaka 20, wengine wakiwa na miaka 70. Vyovyote vile, muhimu ni kujijua wewe mwenyewe, bila ya kujali umefanikisha hilo ukiwa na miaka mingapi.

Unapojijua, ndipo unapoyaishi yale maisha ya kweli. Ambayo unaona kipo kitu unatoa kwa wengine, upo mchango mkubwa unaotoa kwa wengine, na hata kama hakuna anayekulipa kwa kufanya hivyo, hujali. Hili ndiyo linapelekea wewe ufanye kwa ubora zaidi na kuweza kupata matokeo makubwa zaidi.

Kaa chini na wewe, siyo siku moja, bali kila siku. Tafakari maisha yako, ulipotoka, ulipo na unapokwenda. Hii ni njia nzuri ya kuwasiliana na wewe binafsi na kuona wazi wewe ni nani na upo hapa kufanya nini.

Hata kama tayari umeshajijua wewe mwenyewe, mkutano wako na wewe wa kila siku unapaswa kuendelea kuwepo. Maana bila ya hivyo, kelele za dunia zitakusahaulisha na utarudi tena nyuma.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

2 thoughts on “UKURASA WA 968; Kitu Pekee Ambacho Huwezi Kufundishwa Na Yeyote…

  1. Yusuph Hashim

    Kiukweli kabisa wewe ni mmoja kati ya watu wanaonishawishi katika uandishi wako, na unaandika vitu facts kabisa na vinavyogusa kiukweli. Na nina amini watu ambao wanaozikubali kazi zako ni wengi sana, sema wengi wao huwa hawaleti mrejesho kwa kukomenti ama kureply, bali wanayafanya katika matendo na yanawasaidia sana

    Ahsante kaka.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.