UKURASA WA 975; Unamwangalia Nani?

By | September 1, 2017

Kwenye maisha yetu, kuna watu ambao tunawaangalia, watu ambao wanatupa hamasa ya kupiga hatua zaidi kwenye lolote ambalo tunafanya.

Hawa ni watu ambao kwa viwango vyao na mambo waliyofanya, wanatuhamasisha na sisi kuweka juhudi zaidi ili kuweza kufanya makubwa.

Hawa ni watu ambao wanatupa uhakika ya kwamba inawezekana na tunapokutana na changamoto, tunakumbuka kwamba wengine nao wamepita mpaka kufika walikofika.

IMG-20170726-WA0003

Kila mtu kuna mtu au watu anaowaangalia. Hili huwa kuna wanaojua na wasiojua.

Wale wanaowafuata watu bila ya kujua, hujikuta wanafanya mambo ambayo hata hawajui kwa nini wanafanya. Wanajikuta wakifanya kwa sababu ndivyo kila mtu anafanya. Na kwa kuwa hawajachagua wenyewe, hawawezi kufanya makubwa.

Lakini wale ambao wanachagua wenyewe ni watu gani wa kuwaangalia, huwa wanachagua watu bora kabisa, ambao wameweza kufanya makubwa na hivyo kuhamasika kufanya makubwa zaidi.

Chagua mtu au watu ambao mwenendo wao wa maisha, maneno yao na hata matendo yao yanakuhamasisha na kukupa nguvu ya kupiga hatua zaidi. Tumia mtu au watu hawa kama kipimo chako cha kupambana zaidi. Lengo siyo tu kuwashinda au kuwafikia, bali kuwa bora kadiri ya uwezo wako, huku ukiwa na uhakika kwamba hilo linawezekana, kama ambavyo imewezekana kwao.

SOMA; UKURASA WA 713; Jiambukize Mafanikio…

Unaweza kuchagua mtu wa karibu na aliye hai, ambaye utajifunza zaidi kwake kwa kuweza kumfikia na kumfuatilia. Lakini pia unaweza kuchagua mtu ambaye hayupo hai, au aliyepo mbali. Huyu utajifunza kupitia historia ya maisha yake, ambayo utaisoma katika maeneo mbalimbali.

Muhimu hapa ni yule unayemwangalia, uwe umemchagua wewe mwenyewe, kwa vigezo ambavyo ni muhimu kwako, kulingana na ndoto ambazo unakuwa nazo wewe mwenyewe.

Usiende tu kama vile unabahatisha, bali kuwa na mtu unayemwangalia, ambapo ukikwama, unapata hamasa kutoka kwake.

Japo hamasa ya kwanza na ya muhimu kabisa inatoka ndani yako, lakini pale unapoona wengine ambao wamefanya, inakusaidia usikate tamaa, hata kama mambo ni magumu kiasi gani.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.