UKURASA WA 1010; Hasira Za Kurushiwa…

By | October 6, 2017

Wapo watu ambao wana hasira na maisha yao, lakini hasira hizi hawazielekezi kwao wenyewe, bali kwa wengine.

Hivyo kuna wakati unaweza kushangaa mtu anakuwa na hasira na wewe, wakati hakuna jambo lolote baya umemfanyia.

Labda tu umemweleza maendeleo yako mazuri, ghafla anabadilika, anaanza kuwa na hasira na wewe na kukukatisha tamaa kwenye mambo hayo, au kukuonesha wapi unakosea.

Mbaya zaidi, watu wa aina hii wanakuwa ni watu wa karibu sana, watu uliotegemea wangekuwa wa kwanza kukuunga mkono na kufurahia hatua ulizochukua.

Huu ni ukweli mchungu ambao unapaswa kuujua. Kwamba kuna wakati watu watakurushia hasira zao wenyewe, kuzielekeza kwako wakati wewe hujawafanyia jambo lolote baya.

Kuna watu watakasirika na kujisikia vibaya, pale wewe unapochukua hatua ya kuondoka kwenye mambo ya kawaida na kuanza safari ya mafanikio. Pale unapoacha kufanya kile walichozoea kufanya na wewe, na kuamua kuwa bora.

Wengine watakuambia umebadilika sana, wengine watakuambia unaringa na wengine watakuambia unapoteza muda wako bure kwa yale mapya ambayo unafanya.

SOMA; UKURASA WA 283; Dawa Ya Hofu, Wivu, Chuki Na Hisia Zote Hasi…

Jambo la kushangaza zaidi, wapo ambao mwanzo watakupa moyo kwa hatua unazochukua, lakini unapoanza kufanikiwa unashangaa wanabadilika, wanaanza kuwa na hasira na wewe, wanakupinga.

Hii ni kwa sababu walijua hutafika mbali, na mwanzoni hawakutaka waonekane wabaya, ila wanapoona hushindwi, wanapata hasira.

Sasa, hasira zote hizi ambazo watu wanazileta kwako siyo kwa sababu yako (labda kama umewafanyia ubaya), ila mara nyingi ni kwa sababu zao. Wewe unapoweza kufanya makubwa wakati wao hawafanyi, inawafanya wajisikie vibaya. Lakini hawapo tayari kukiri kwamba kinachowazuia kufanya ni uzembe wao wenyewe.

Hivyo wanataka kila mtu abaki vile alivyo, ili uzembe wao usionekane.

Wajue watu wa aina hii kwenye maisha yako, hii itakusaidia kuwaepuka, kuepuka kuwaeleza kila hatua unayofanya na hiyo itapunguza mikwaruzo isiyo ya msingi.

Na muhimu zaidi; USIWE MTU WA AINA HII. Kama yupo mtu ambaye mlikuwa sawa, lakini sasa hivi unaona anafanya vizuri, anakuacha nyuma, usikasirike wala kumchukia, badala yake mpende, mfuatilie kwa karibu, jifunze kipi anafanya anakuwa bora ili na wewe uchukue hatua na kuwa bora zaidi.

Usiwachukie watu kwa sababu wanapiga hatua na kukuacha wewe nyuma. Na wala usijichukie wewe mwenyewe kwa sababu wengine wanapiga hatua na wewe unabaki nyuma. Chuki ni sumu, chuki haitakuachia uchukue hatua. Wapende wote wanaofanikiwa na jifunze kutoka kwao, chukua hatua ili na wewe pia ufanikiwe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.