UKURASA WA 973; Usiangalie Nje Pekee, Angalia Misingi…

By | August 30, 2017

Napenda kitu kimoja muhimu kuhusu misingi, na kitu hicho ni kwamba, misingi huwa haibadiliki, ije mvua lije jua, misingi inaendelea kuwa misingi.

Ndiyo maana ukiangalia watu wote ambao wamefanikiwa kwenye maisha, ipo misingi ambayo wanaifuata na kuiishi. Hawaendi tu kama bahati kwa kujaribu mambo na kuona yanaendaje. Badala yake wanajua nini wanafanya na wanategemea kupata nini.

Misingi huwa haimwangushi yeyote anayeifuata, japo changamoto zipo, lakini misingi inamweka mtu upande salama.

Kufuata misingi pia kuna changamoto zake, kuna wakati kufuata kwako misingi kutakunyima vitu vizuri, ambavyo wengine wanavipata. Lakini hilo huwa ni la muda tu. Kwa kipindi kirefu, misingi inakusaidia zaidi.

Chochote unachotaka kufanya au kushawishiwa kufanya, angalia kwanza misingi. Hata kama watu wanakushawishi kiasi gani, hata kama watu wanakuambia wamenufaika sana, angalia kwanza misingi, je ipo sawa. Kama ipo sawa, ingia na fanya. Kama misingi haipo sawa, usiingie, hata kama dunia nzima inakazana na kitu hicho.

Nakukumbusha hili rafiki kwa sababu watu wengi wametapeliwa na kujiingiza kwenye biashara ambazo siyo sahihi kwao na hazifuati misingi ya biashara. Kilichowasukuma kuingia ni baada ya kuoneshwa kwamba wengine wamepata fedha. Wanaona kabisa kwamba msingi siyo sahihi, lakini kwa kuwa wengine wananufaika, wanaona siyo vibaya nao kunufaika.

Kweli unaweza kunufaika na fedha za muda mfupi, lakini kwa muda mrefu ukaharibu jina lako, sifa yako na hata uaminifu wako. Unaweza kupata fedha leo halafu kesho kila mtu akawa anakunyooshea kidole. Au ukaogopa kusimama mbele ya watu kama mfano mzuri wa mafanikio.

Ijue misingi muhimu kwenye kila eneo la maisha yako, na hakikisha unaiishi misingi hii kila wakati. Usifanye lolote ambalo linakwenda kinyume na misingi ya eneo husika, hata kama utanufaika, haitakuacha salama.

Misingi haivunjwi wala kumwonea yeyote huruma, ivunje na yenyewe itakuvunja.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA tuna msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, huu ni msingi muhimu wa maisha ya mafanikio, ambao unatuwezesha kufanya makubwa sana.

SOMA; PESA NA BIASHARA; Misingi Mitatu Muhimu Ya Kuifuata Ili Kuwa Na Biashara Yenye Mafanikio.

Misingi mingine unaweza kuitengeneza kulingana na mipango yako na hata mazingira yako.

Kwa mfano;

Biashara; msingi wa biashara ni mabadilishano ya thamani, usiangalie faida pekee, angalia thamani gani unatoa kwa wengine.

Fedha; msingi wa fedha ni kuizalisha zaidi, hivyo kwa kila kipato ambacho unatengeneza, hakikisha kuna sehemu ya kipato hicho unaitumia kuzalisha kipato zaidi. Usitumie fedha yote unayoipata.

Kazi; msingi wakazi ni kuongeza thamani kwa wengine, kutoa mchango kwenye dunia. Usifanye kile ambacho kinawaumiza wengine.

Mahusiano; msingi wa mahusiano ni kuaminiana na kujaliana, wajali wale ambao ni wa muhimu kwako, na mahusiano yatakuwa imara.

Misingi ipo mingi, chagua ile inayoendana na wewe na hakikisha unaiishi. Jambo lolote unalotaka kufanya, hasa jipya kwako, chukua muda wa kuijua misingi kwanza kabla hujafanya maamuzi. Kwa sababu wengi wamekuwa wanakimbilia kufanya kabla hawajaijua misingi, na hilo limekuwa linawaumiza.

Ifuate na kuiishi misingi, utajiepusha na changamoto zisizo za lazima kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.