UKURASA WA 1017; Acha Kufanya Kazi, Anza Kuzalisha…

By | October 13, 2017

Siku za nyuma kidogo, kuna rafiki yangu alikuwa ndiyo ameajiriwa kwa mara ya kwanza. Alipofika kazini alikuwa na hamasa kubwa ya kufanya kazi. Akatumwa kwenda mkoa fulani kikazi, alipofika kule alipanga kufanya kazi hiyo na kuikamilisha haraka ili arudi eneo lake la kazi.

Alipoanza ufanyaji wake wa kazi wa kasi ili kumaliza mapema, watu ambao walikuwa wazoefu zaidi kwenye kazi ile walimwita pembeni, wakamuuliza mbona ana haraka sana? Aliwaambia anataka amalize kazi mapema arudi. Watu wale wakamwambia watu huwa hawafanyi kazi ili iishe mapema, bali wanafanya kazi ili kesho kuwe na kazi nyingine ya kufanya. Na wakazidi kumshangaa, kwa nini ukimbilie kumaliza, badala ya kuvuta kazi ili uendelee kulipwa zaidi kwa kuwa nje ya kituo chako cha kazi?

Katika mfano huu unaweza kuona sehemu mbili hapo kuhusiana na kazi. Kuna upande wa kufanya kazi, kuonekana upo kazini na unafanya kazi na kuna upande wa kuzalisha, kutoa matokeo ambayo yanategemewa.

Ukiangalia kwa kina, watu wengi wanakwama kwa sababu wanafanya kazi na hawazalishi. Wanachokazana kufanya ni kuonekana wapo kazini, wanafanya kazi, lakini kwa uhalisia hakuna kikubwa wanachozalisha.

Wengi wanafanya kazi kiasi cha kuonekana wamefanya kazi na hawafikirii kama wamezalisha matokeo yaliyokuwa yanategemewa.

Lakini hivi sivyo watu wanaofanikiwa wanavyochukulia kazi zao, hawachukulii kama kazi tu na kufanya ili waonekane, bali wanachukulia kama mradi ambao wanahitaji kupata matokeo fulani.

Wanachoangalia ni matokeo wanayozalisha, na hilo linawafanya kuwa na ufanisi mkubwa, kwa kuzingatia yale ambayo ni muhimu, tofauti na wale wanaofanya ili waonekane wanafanya kazi.

Ndiyo maana nakuambia ACHA KUFANYA KAZI NA ANZA KUZALISHA, anza kutoa matokeo, anza kufikiria njia bora za kufanya kazi zako ili kuweza kupata kile unachotaka kupata.

Usifanye ili uonekane na wewe unafanya, bali fanya ili kuzalisha matokeo makubwa na ya tofauti, yanayowasaidia wengine. Na hapo ndipo mafanikio makubwa yalipo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.