UKURASA WA 900; Maisha Yako Ni Kazi Inayoendelea….

By | June 18, 2017

Kabla hujapata chochote ambacho unakitaka sana, huwa unafikiri ukishakipata basi ndiyo umemaliza kila kitu. Lakini unapokipata ndiyo unagundua kumbe ni mwanzo kabisa wa maisha kuwa bora kwako.

Mfano kabla hujamaliza masomo, unaona ukimaliza masomo basi ndiyo umemalizana na changamoto. Lakini unapomaliza ndiyo unagundua unahitaji kujifunza zaidi hata ya ulivyokuwa unajifunza wakati upo masomoni.

Au kabla hujapata kazi unajiaminisha ukipata kazi basi changamoto zako za kifedha ndiyo zimeisha. Lakini unaipata na kugundua kwamba changamoto za fedha ndiyo zinakuwa nyingi zaidi hata ya awali.

Kabla hujaanza biashara unajiaminisha kwamba ukishakuwa na biashara tu, basi maisha yako yamekuwa mazuri. Hakuna wa kukupangia ufanye nini na hakuna wa kukupangia ulipwe kiasi gani. Ni mpaka uingie kwenye biashara ndipo unagundua changamoto ni nyingi, kuna wateja wasumbufu na hata kipato, kinatofautiana kutokana na mambo mbalimbali.

SOMA; Wewe Ni Kazi Ya Sanaa…

Kwa chochote tunachofanya, au tunachotaka sana kwenye maisha yetu, tunapaswa kuacha kuwa na matumaini hewa. Tuache kujidanganya kwamba tukishapata kile tunachokazana kupata, basi mambo yote yatakuwa safi.

Maisha yetu ni kazi inayoendelea, au kama wanavyosema kwa Kiingereza, WORK IN PROGRESS. Hakuna hatua moja ambayo tukishaifikia kazi imekamilika. Unakazana na kufika pale unataka kufika na ndipo unapozikuta changamoto mpya ambazo hukuzijua.

Hivyo rafiki yangu, jikumbushe hili mara zote, kujidanganya kwamba mambo yatakuwa poa kwa kufika pale unapokazana kufika, ni kujiandaa kuangushwa. Wewe jua ni kazi inayoendelea, ukifika unakokazana kufika sasa, kuna mengine muhimu ya kufanyia kazi. Kila siku mpya inakuja na mambo yake mapya. Na yote yapo kwenye uwezo wako wa kuyafanyia kazi, iwapo utayaelewa vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.