UKURASA WA 1000; Siku Elfu Moja (1000) Za Kuandika Kila Siku Bila Ya Kuacha Hata Siku Moja.

By | September 26, 2017

Habari za leo rafiki yangu?

Lao Tzu aliyekuwa mwanafalsafa wa china amewahi kunukuliwa akisema safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja. Hichi ndicho kilichotokea tarehe 01/01/2015 ambapo safari ya kuandika makala za KURASA kila siku ilianza, na tangu siku hiyo sijawahi kuacha hata siku moja bila ya kuandika. Mpaka kufika leo siku ya 1000. Nimejifunza mengi katika safari hii, leo ninapenda nikushirikishe yale muhimu sana.

Vitabu

Lakini kabla ya kukushirikisha hayo, nianze kukushirikisha wazo hili la makala za kurasa lilikujaje.

Nimekuwa naandika tangu siku nyingi, japokuwa sikuwahi kuwa na mfumo wa kuandika mara kwa mara. Kabla ya mwaka 2012 nilikuwa naandika tu kama kujifurahisha au kukosoa vitu fulani, na nilikuwa nafanya hivyo zaidi kupitia mitandao ya kijamii. Mwaka 2012 nilikuwa naandika vitu mbalimbali, lakini nilihama kutoka kwenye ukosoaji na kujaribu kuandika vitu mbalimbali. Mwaka 2013 nilianza kuandika rasmi kama kazi yangu, yaani sikuwa tena naandika kukosoa au kufurahia, bali nilichagua kuandika kama kazi yangu rasmi. Hapa ndipo nilipoanzisha mtandao wa AMKA MTANZANIA na baadaye KISIMA CHA MAARIFA.

Tangu kipindi chote hicho, nimekuwa naandika mara nyingi, kwa mfano mwaka 2013 na mwaka 2014 nilikuwa naandika mara nyingi, kuna siku nilikuwa naweza kuandika makala hata tano, siku nyingine nisiandike. Pamoja na kufanya uandishi kuwa kazi yangu, bado sikuwa na utaratibu wa kuandika kila siku. Siku nikiamka sijisikii vizuri basi ilikuwa sababu nzuri ya kutoandika, siku nikiamka najisikia vizuri naandika makala nyingi.

Katika kipindi hicho nilikuwa natamani sana nipate mfumo wa kuniwezesha kuandika kila siku, bila ya kujali najisikiaje, bila ya kujali nipo wapi.

Siku ya mwaka mpya tarehe 01/01/2015 nakumbuka nilikuwa kwenye kivuko cha kwenda kigamboni nikiwa na familia tukienda kwenye mapumziko, uliingia ujumbe kwenye simu yangu. Ulikuwa ni ujumbe wa kunitakia heri ya mwaka mpya, zile aina ya jumbe ambazo watu hutengeneza na kutuma. Lakini ujumbe huu ulikuwa wa tofauti na zile nyingi nilizopokea. Ujumbe huu ulisema leo ni mwaka mpya, ni ukurasa mpya wa mwaka 2015, wewe ndiye utakayeamua uandike nini kwenye ukurasa huu na kurasa nyingine za mwaka huu.

Ujumbe huu ulinifanya nifikiri tofauti, kumbe kila siku mpya tunayoianza ni ukurasa mpya wa maisha yetu. Na hapo ndipo nilipopata wazo la kuwa na makala hizi za kurasa, ambapo kila siku nitaandika makala yenye urefu wa ukurasa mmoja wa kitabu. Makala hizi hazitakuwa na ajenda maalumu, bali zinakuwa ni zenye funzo na hatua ambazo mtu unaweza kuchukua na kuyafanya maisha yako kubwa bora zaidi.

Siku hiyo hiyo usiku niliandika ukurasa wa kwanza na kuhakikisha inaenda hewani. Hivyo nilijiwekea utaratibu wa kuandika kila siku makala hizi za kurasa, na makala nyingine pia, bila ya kuruka hata siku moja.

Nafurahi sana leo nimefika ukurasa wa elfu moja, siku elfu moja za kuandika kila siku, bila ya kuruka hata siku moja. Ni safari ambayo nimejifunza mengi sana, lakini kubwa kuliko yote ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA.

Kuandika kila siku kunahitaji NIDHAMU ya hali ya juu. Kuna siku unaweza kuamka hujisikii vizuri, siku nyingine unaamka unaumwa, siku nyingine unaamka haupo kwenye mazingira mazuri, lakini yote hayo sikuruhusu yawe sababu, badala yake nilihakikisha kila siku naandika.

Bila ya UADILIFU ni vigumu sana kuweza kuandika kila siku. Kwa teknolojia tunayotumia, ni rahisi kudanganya kwamba unaandika kila siku. Kwa mfano, naweza kuandika leo, lakini nikapanga nilichoandika kiende hewani siku ya kesho. Lakini sikuwahi kujaribu kufanya hili. Niliendelea kusimamia utaratibu wa ukurasa wa siku husika nitaundika kwenye siku husika. Ninajua kabisa hata nikidanganya kwamba nimeandika kila siku wakati kuna siku niliandika kwa ajili ya siku nyingine, hainiongezei chochote na zaidi nitakuwa nimejidanganya mwenyewe, na hilo litaishi na mimi milele, kwamba nilidanganya naandika kila siku na sijafanya hivyo. Huu ndiyo uadilifu, umenisaidia sana kwenye hili.

Hakuna kilichoniwezesha kuandika siku hizi elfu moja kama KUJITUMA. Katika siku hizi elfu moja, kuna kipindi nimesafiri maeneo ambayo mtandao ni wa shida, umeme hakuna na safari inakuwa a uchovu wa hali ya juu. Lakini sikuruhusu hayo yote kuingilia utaratibu wangu. Nikiwa kwenye baadhi ya safari, ilikuwa inanibidi niende umbali mrefu kupata mtandao au umeme wa kuhakikisha naandika kwa siku husika. Nimekuwa na line za mitandao yote ya simu na ninatembea nazo popote, nikifika eneo line ya aina moja ikisumbua, naulizia ni ipi huwa inakubali maeneo hayo na ninaitumia. Muda wote ninahakikisha nimebeba vocha za ziada, ili kifurushi cha intaneti kisiishe halafu niwe sina jinsi ya kuongeza kifurushi kingine.

Kikubwa sana ninachoweza kukuambia rafiki yangu ni hichi, kama ningeanza kwa kusema nataka niandike siku elfu moja kila siku, huenda ningeona ni zoezi gumu kabisa na lisilofaa. Lakini niliposema nitaandika kila siku, na siku inapofika naandika, linakuwa zoezi rahisi zaidi.

Kingine kikubwa sana ni kwamba ukitafuta sababu unaipata. Ukitaka sababu ya kufanya kitu utaipata na ukitaka sababu ya kutokufanya kitu pia utaipata. Sababu hazijawahi kukosekana. Kuna nyakati nimekuwa napata sababu nyingi za kwa nini nikiacha siku moja siyo mbaya, lakini inakuja sababu kubwa zaidi ambayo ni napaswa kuandika kila siku, na hapo nakaa chini na kuandika.

Ninashukuru kwa siku hizi elfu moja zilizopita sijapata changamoto kubwa ambayo ingeweza kuathiri utaratibu wangu wa kuandika kila siku. Na ninaposema changamoto kubwa namaanisha kitu kama kuumwa kunakopelekea kulazwa hospitali, au ajali kubwa inayoweza kupelekea kushindwa kuandika. Lakini nina imani hata ikitokea changamoto kubwa kiasi gani, kama nipo hai, nitahakikisha kila siku naandika makala hizi za kurasa. Hata kama mikono itashindwa kuandika, basi nitamweleza mtu anisaidie kuandika, nimsimulie na yeye aandike.

Makala hizi za KURASA zilianza kupatikana kwenye blog ya MAKIRITA AMANI, baadaye nilifunga blog ile na kuzihamishia kwenye KISIMA CHA MAARIFA, zikawa kwenye kipengele cha bure, baadaye zikawa kwa wale waliojiunga. Sasa hivi nazirejesha makala hizi kwenye kipengele cha kuzisoma bure, hivyo yeyote yule ataweza kusoma makala za kurasa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, iwe amejiunga au hajajiunga.

Karibu kwenye KURASA KUMI ZA KITABU.

Rafiki, nimeanza program nyingine mpya ya KURASA KUMI ZA KITABU KILA SIKU. Nimekuwa nasoma vitabu kwa muda mrefu, lakini nimeanza kusoma vitabu kwa wingi tangu mwaka 2012 na zaidi mwaka 2013. Mwaka 2014 tulianzisha kundi la TANZANIA VORACIOUS READERS ambapo kila wiki tunasoma vitabu viwili, na kwa mwaka vitabu 100. Tumeshasoma vitabu zaidi ya 200 kwenye kundi hili. Lakini ni kundi ambalo lina masharti makali sana. watu wengi waliojiunga hawakufanikiwa kukaa muda mrefu, kwa sababu usiposoma kitabu unaondolewa.

Watu wengi wamekuwa wananiambia kwamba wanapenda sana kusoma vitabu, ila muda ni changamoto, kazi zao zinawabana na hawapati kabisa muda wa kusoma. Nimekuwa nawashauri wasome kurasa 10 tu kwa siku kila siku, na kwa mwezi watamaliza kusoma kitabu kimoja. Kitu ambacho kitawafanya kuwa mbele zaidi ya wengine. Wanaanza siku chache lakini baadaye wanaacha.

Nimeanzisha program ya kurasa kumi za kitabu kila siku, ili kuwasaidia watu kujenga nidhamu ya kusoma kurasa kumi tu za kitabu kila siku. Hiyo ni kila siku, unatenga muda, unakaa chini na kusoma kurasa 10, kisha unaandika maelezo ya aya moja ya kuelezea ulichojifunza kwenye kurasa kumi ulizosoma na hatua unazokwenda kuchukua. Kisha unatushirikisha hilo kwenye kundi maalumu la kusoma kurasa hizi kumi.

Kitabu unachosoma unachagua wewe mwenyewe, na kama hujui au huna kitabu cha kusoma, nitakushauri baadhi ya vitabu unavyoweza kusoma. Pia kila mwezi nitakuwa napendekeza vitabu vya kusoma kwa maeneo ya biashara, uongozi, fedha, mafanikio na hamasa.

Kama ungependa kuingia kwenye kundi hili, basi nitumie ujumbe kwenye wasap namba 0755 953 887 ukiwa umeandika PROGRAM YA KUSOMA KURASA KUMI, nitakutumia maelekezo. Kabla hujatuma ujumbe huo, jua kwamba lazima usome kila siku, la sivyo unaondolewa, na kila mwezi utalipa ada ya tsh 10,000/= ambayo haitarudishwa hata kama umeondolewa kabla ya mwezi kuisha.

Najaribu kukujengea mazingira yatakayokusukuma kujijengea nidhamu kubwa sana ya usomaji na mambo mengine pia. Na ninategemea kundi hili likue zaidi kwa nidhamu zaidi ya usomaji na mambo mengine pia. Hivyo karibu sana. tuma ujumbe kwenye wasap 0755 953 887 wenye maneno PROGRAM YA KUSOMA KURASA KUMI na nitakutumia maelekezo.

Rafiki, nimalize kwa kukukumbusha msingi wetu wa maisha ya mafanikio ambao ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, kazana kuishi kwa vitu hivyo vitatu kila siku, na yale unayoona hayawezekani, yatawezekana.

Karibu tuendelee kuwa pamoja kila siku, tukijifunza na kuwa bora zaidi ili kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

2 thoughts on “UKURASA WA 1000; Siku Elfu Moja (1000) Za Kuandika Kila Siku Bila Ya Kuacha Hata Siku Moja.

  1. Pingback: UKURASA WA 1012; Vitu Viwili Utakavyoenda Navyo Kaburini… – Kisima Cha Maarifa

  2. Pingback: UKURASA WA 1097; Miaka Mitatu Ya Kurasa Na Nguvu Ya Kufanyia Kazi Wazo… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.