UKURASA WA 863; Kila Kitu Kinarudi Kwenye Asili Yake…

By | May 12, 2017

Kama una maji ambayo yamechanganyikana na mtope, ukiyaacha kwa muda, matope yote yatatulia chini na maji yatabaki kuwa safi kabisa, bila uchafu wa aina yoyote ile. Hapo hujafanya wala kuongeza chochote, bali umeyaacha maji yakatulia yenyewe. Inakuwa hivyo kwa sababu asili ya maji ni masafi, maji kwa asili hayajachanganyikana na matope, hayo yamekuja tu baadaye, hivyo maji yanapotulia, tope hujitenga na usafi hubaki.

Kadhalika kwenye akili zetu, kuna wakati tunakuwa tumevurugwa na mengi, na kuona kama hatuwezi kutuliza akili zetu. Mawazo mengi, msongo wa mawazo na kila aina ya kelele. Wakati kama huu unaweza kuona kama huwezi kabisa kuondokana na kelele hizo. Lakini asili ya akili ni utulivu, hivyo unapotulia, mawazo na kelele zote zinaondoka na kuiacha akili kwenye asili yake.

SOMA; kuishi kama asili ilivyopanga.

Wengi wameshindwa kuzituliza akili, kwa sababu wakati zimechanganyikana na kelele, wanachofanya ni kuongeza kelele zaidi. Yaani ni sawa na maji yana matope, halafu wewe unaendelea kuyatikisa zaidi. Yanazidi kuvurugika na huwezi kupata usafi wake.

Hivyo pia kwenye kupata usafi na utulivu wa akili, lazima uzitenge kelele. Lazima kwa makusudi uzuie mawazo yoyote kuingia kwenye akili yako, na kuiacha itulie kabisa. Hapo utaweza kuirudisha kwenye asili yake, utaweza kufikiri kwa usahihi na kuona hatua sahihi kwako kutulia.

Hili ni jambo muhimu sana kufanya kila siku, hasa kwa dunia ya sasa ambayo imejaa kila aina ya kelele. Ambapo ukishika tu simu yako, dunia nzima inakurushia kila aina ya kelele. Kila siku, pata muda wa kuifaidi akili yako ikiwa imetulia. Akili hii itakuwezesha kutatua changamoto yoyote unayopitia, itakuwezesha kuziona fursa ambazo wengi hawazioni.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.