UKURASA WA 876; Kuhusu Kupambana, Kushindana Na Kubishana…

By | May 25, 2017

Dunia haitakuacha ufanye chochote unachotaka bila ya kukusumbia, hivyo kuna wakati unahitaji kupambana, kushindana na kubishana.

Mapambano hayo inabidi yawe kwenye kile unachofanya, na siyo kwa watu. Kwa sababu, kupambana, kushindana na kubishana na watu, kunakuwa na madhara makubwa kwako wewe mwenyewe, hata kama utashinda.

Lakini watu hawatakuacha hivi hivi, hata kama utaamua kujali yako, wapo ambao wataacha yao na kuanza kujali yako, kuanza kukufuatilia, kukusumbua kwa lolote unalofanya. Inafika wakati kuwaacha waendelee kufanya hivyo kunaharibu sifa yako na hata mipango yako ya baadaye, hivyo unahitaji kuchukua hatua.

Hapo ndipo unaweza kupambana nao, kwa kuhakikisha unawazuia kuendelea kufanya kile wanafanya. Kushindana nao, kuhakikisha hawachukui kirahisi kile ulichonacho na hata kubishana nao kuhakikisha hawabadili kile unachosimamia.

Changamoto ni kwamba, watu wengi wanaoingia kwenye hayo mapambano, mashindano na mabishano na watu, huwa hawajui wapi pa kuishia na hivyo kujikuta wakitumia muda wao mwingi kwa wengine badala ya mafanikio yao binafsi.

Hapa nimekuletea mwongozo mfupi sana wa kutumia unapofika kwenye hali kama hii, ili uepuke kupoteza muda na uweze kufanikiwa.

SOMA; Njia Ya Kupambana Na Maisha Magumu.

Kuhusu kupambana.

Kwanza usipambane na mtu yeyote yule, inakupotezea muda. Lakini kama mtu atasisitiza mapambano, yaani atakuwa anakusumbua na inabidi uchukue hatua, basi inabidi upambane. Ila zingatia haya mawili;

Moja; hakikisha unashinda kabisa pambano unaloanzisha, usiishie njiani, maliza kabisa pambano unaloingia.

Mbili; hakikisha unatumia muda mfupi, gharama ndogo na rasilimali chache kwenye pambano lolote, ili usikose vya kutumia kwenye mafanikio yako.

Kuhusu kushindana.

Muhimu ni usishindane, kwa sababu hakuna chochote unachopata kwenye mashindano zaidi ya maumivu.

Lakini kama ushindani ni mkubwa, njia bora kabisa kwako kushindana ni kuwa bora zaidi ya wengine wote wanaofanya kile unachofanya. Kuwa wa kipekee kabisa, kwa kutoa ambavyo wengine hawawezi kutoa.

Kuhusu kubishana.

Usibishane kwa maneno, bishana kwa matendo. Wakisema wewe fanya, vitendo vinaongea zaidi kuliko maneno.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.