UKURASA WA 853; Njia Ya Kusikika Kwenye Kelele….

By | May 2, 2017

Kelele huwa zinaanzaje? Huwa hazianzi mara moja, kwamba kila mtu anajikuta anapiga kelele. Bali watu wanaanza kuongea kwa sauti ya chini, sasa wanapokuwa wengi wanaongea kwa sauti za chini chini, sauti zinaingiliana na hivyo hawasikilizani vizuri. Hii inapalekea kuanza kuongeza sauti kidogo kidogo ili wasikilizane vizuri. Kadiri wanafanya hivyo ndivyo wanazidi kushindwa kusikilizana, mwishowe inabidi watu wapige kelele zaidi ili kusikilizana.

IMG-20170217-WA0002

Hivyo basi, unapokuwa katikati ya kelele nyingi, njia pekee ya kusikika siyo kupiga kelele zaidi. Kwa sababu ukifanya hivyo, na wengine nao watapiga kelele maradufu, watafunika kabisa sauti yako. Na hata ukisema unapiga kelele kubwa zaidi ambayo wengine hawawezi kuifikia, utakachoondoka nacho ni maumivu ya kichwa.

Njia pekee ya kusikika unapokuwa katikati ya kelele nyingi, ni kujitenga na kelele hizo. Basi, rahisi kama hivyo.

Unahitaji kujiweka pembeni na kelele hizo, mbali kabisa ambapo kelele hazitakufikia, na hapo utaweza kuongea na wale wanaokusikiliza, wakakusikiliza vizuri sana.

SOMA; Watu Wana Matatizo Yao, Hawataki Kusikia Yako….

Kwa jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako, epuka sana kuwa katikati ya kelele. Na kelele tunazosema hapa ni kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla, kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, ni kujiweka katikati ya kelele, hakuna atakayekuona au kukusikia, kwa sababu kelele ni nyingi.

Unaondokaje kwenye kelele?
kwa kujitofautisha, kwa kutafuta kitu ambacho kitawafanya watu watake kuja kwako licha ya kuwepo kwa wengine wengi. Lazima uwe na kitu hichi kwa jambo lolote unalofanya, kwa sababu zama hizi, wengi wanafanya kile unachofanya.

Weka juhudi zaidi, kuwa mbunifu zaidi, ongeza thamani na nenda hatua ya ziada kwenye kila jambo unalofanya. Kitu chochote ambacho unaruhusu mkono wako ushike, basi hakikisha unaacha alama ambayo hakuna mwingine awezaye kuiacha. Hivi ndivyo unavyoweza kujitenga na kelele, ukafanya makubwa na ukafanikiwa sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.